Sababu kuporomoka kwa taaluma zatajwa

22Oct 2020
Neema Emmanuel
MWANZA
Nipashe
Sababu kuporomoka kwa taaluma zatajwa

Imeelezwa kuwa mimba za utotoni, kushuka kwa nidhamu, utoro kwa wanafunzi na wazazi kutofatilia maendeleo yao ni miongoni mwa sababu zinazotajwa kusababisha kuporomoka kwa taaluma mkoani Mwanza.

Sababu hizo zimetolewa leo na Afisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Martine Nkwambi wakati akitoa taarifa ya hali ya elimu mkoani humo katika kikao cha wadau wa elimu mkoani humo.

Amesema kuwa sababu nyingine ni mazingira ya shule kuwa mbali na kuporomoka kwa maadili miongoni mwa walimu.

Amesema wanafunzi wanaojihusisha na masuala ya ngono hukosa umakini katika masomo yao na baadhi huishia kupata mimba hatimaye kuacha shule.

Amesema kwa mujibu wa mamlaka za serikali za mitaa mwaka huu takwimu zinaonyesha katika shule za msingi kuanzia mwaka 2015 hadi 2019 wanafunzi waliosajiliwa ni 462,235 waliomaliza 312,545 huku walioacha wakiwa ni 149,690 na kwa upande wa shule za sekondari kuanzia mwaka 2016 hadi 2019 waliosajiliwa ni 158,257, waliomaliza wakiwa 102,935 na walioacha wakiwa 55,322.

"Walimu baadhi ushiriki udanganyifu kwenye mitihani  ya taifa, kuwatumia wanafunzi kingono, upungufu wa walimu , upungufu wa miundombinu na samani umbali kati ya shule na makazi huchochea wanafunzi kukatisha masomo jambo hilo huongeza tabaka la watu wajinga na wahalifu ,vilevile hushusha asilimia ya ufahulu wa shule na kuvuruga malengo ya Taifa" ameeleza Nkwabi.

Ameongeza kuwa ili kuondokana na adha hizo mikakati mbalimbali ya kupandisha taaluma imeandaliwa ikiwemo kudhibiti utoro na mimba mashuleni kwa kuanzisha vipindi vya dini na ushauri nasaha pamoja na kila halmashauri kuunda Kamati ya Maendeleo ya Elimu Kata (KAMAEKA).

Ametaja mikakati mingine kuwa ni kudhibiti utoro wa walimu na maombi ya ruhusa zisizo na tija, kutopoteza kipindi chochote kwenye darasa, kuwepo kwa program za ufundishaji wa ziada unaozingatia uwezo wa wanafunzi, halimashauri kufanya vikao na maofisa elimu kata na walimu wakuu kila mwezi na kuwepo utaratibu wa kuaminika wa ufatiliaji wa ufundishaji kwenye shule zote zilizopo kwenye kila halmashauri.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Cornel Magembe amesema ni jambo la aibu kila yanapotoka matokeo ya kitaifa na Mkoa wa Mwanza unakuwa upo ndani yote hayo yanasababishwa na ufatiliaji na usimamizi kutokuwa mzuri hivyo aliiagiza ufatiliaji uwe mkubwa ili kuleta maendeleo katika sekta hiyo ya elimu.

Amesema wanafunzi wote wanaomaliza darasa la saba wawe wanajua KKK tatu ambazo ni kusoma, kuandika na kuhesabu huku waliopo sekondari wasimalize kwa kupata daraja sifuri kinyume na hapo kiongozi yeyote aliyewasimamia wanafunzi hao watawajibishwa.

Habari Kubwa