Sababu maambukizi ya VVU kushuka Dar

03Dec 2018
Gwamaka Alipipi
Dar es Salaam
Nipashe
Sababu maambukizi ya VVU kushuka Dar

MAAMBUKIZI ya Virusi vya Ukimwi katika Mkoa wa Dar es Salaam yameshuka kutoka asilimia 10.9 mwaka 2015 hadi asilimia 4.7 mwaka huu.

 

Mganga Mkuu wa Dar es Salaam, Dk. Grace Maghembe, aliyasema hayo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, kwa mkoa wa Dar es Salaam yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mavulunza yakiwa na kauli mbiu ‘Pima, Jitambue, Ishi’.

“Maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi katika mkoa wa Dar es Salaam yameendelea kushuka kwa kasi kwa kipindi cha miaka minne, kwa asilimia 6.2 kutoka mwaka 2015 hadi 2018,” alisema Dk. Maghembe.

Alisema hali hiyo imetokana na mkoa wa Dar es Salaam kulivalia njuga suala la maambukizi ya VVU, kwa kuhamasisha watu kujitokeza kupima.

Alisema uhamasishaji wa kupima VVU katika Mkoa wa Dar es Salaam umeelekezwa zaidi kwa wajawazito, wanaume pamoja na wananchi wa kawaida.

Alisema serikali pia imeongeza vituo vya kutolea dawa za kufubaza VVU, na kwamba kwa sasa idadi imefikia vituo 180 kutoka 30 miaka ya nyuma.

“Tumefanya jitihada kubwa katika uhamasishaji wa wananchi kujitokeza katika upimaji wa Virusi vya Ukimwi, na mwitikio umekuwa mkubwa,” alisema Dk. Maghembe.

Alisema pia wamekuwa wakitoa elimu shuleni, kushirikiana na taasisi zinazopamba na maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi kwenye kutoa elimu kwa watu walioathirika wasiweze kupata maambukizi mapya, wala wasiweze kuwaambukiza watu ambao hawajaathirika.

“Kwa siku ya leo wananchi asilimia 80 wamejitokeza kupima, na kampeni hii itakuwa endelevu na pia watu watambue kuwa asilimia 50 ya wagonjwa wa kifua kikuu wanaishi na virusi vya Ukimwi,” alisema Dk. Maghembe.

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alisema mkoa huo unatarajia kuendesha operesheni kwenye madangulo ya kuwaondoa wasichana wanaouza miili yao maarufu  ‘machangudoa’.

Naye Mratibu wa Taifa wa Mapambano ya Kifua Kikuu na Ukimwi Temeke (Mukikute), Retcho Jackob, alisema wamekuwa wakihamasisha wananchi kujitokeza kupima tangu mwaka 2005.

 

 

Habari Kubwa