Sababu mwizi kusinzia baada ya kuiba kwa Farouk Karim wa ITV

02Jun 2020
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
Sababu mwizi kusinzia baada ya kuiba kwa Farouk Karim wa ITV

Mwandishi wa Habari wa ITV Visiwani Zanzibar, Farouk Karim amesema hakuna mtego wowote alioweka katika gari lake baada ya kijana mmoja aliyetambulika kwa jina la Daudi Suleiman maarufu Kiboko amekutwa amelala ndani ya gari hilo wakati akiwa katika harakati za kutekeleza uhalifu.

Amesema kuwa siri kubwa ambayo mtu yeyote anaweza kuifanya ili wezi watakapofika nyumbani kwake waibe lakini wapitiwe na usingizi hapo hapo ni kumuamini na kumuomba Mungu ili awalinde wote ndani ya familia.

“Mimi sina dawa yoyote niliyotumia Mungu tu kataka kumuadhirisha kijana huyo ambae ni mwizi maarufu hapa mtaani kwetu Fuoni,” amesema 

Akizungumza na The Guardian Digital, Farouk, amesema kuwa baada ya mwizi kuruka geti la nyumba yake huko Fuoni visiwani Zanzibar na kuiba nguo na viatu lakini baadaye aliingia ndani ya gari na kupitiwa usingizi. 

"Huyu mwizi kaingia usiku wa manane karuka geti, na hatuna mlinzi pale nyumbani, kakusanya zile nguo zilizokuwa zimeanikwa kaziwekwa kwenye mfuko, katika magari yaliyokuwepo pale gari moja lilikuwa wazi akaingia, akapitia mlango wa abiria akachukua power window, akaenda upande wa dereva kuchukua power window ikamshinda ndiyo akalala hapo hapo" amesema Farouk Karim.

Ameeleza kuwa kijana huyo kwa sasa anashikiliwa na jeshi la polisi kwa hatua zengine za kisheria.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jana Juni 1,2020 Jumatatu ambapo kijana huyo akiwa na vitu mbalimbali alivyoviiba ndani ya nyumba ya Farouk alinasa katika gari hilo na kulala usiku kucha bila ya kutarajia.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharib Unguja, Saimon Pasua, amesema jeshi la polisi linamshikilia kijana huyo na uchunguzi na utakapokamilika atafikishwa Mahakamani hatua zaidi za kisheria.

Habari Kubwa