Sababu vifo majeruhi ajali ya Lori Moro kuongezeka yatajwa

21Aug 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Sababu vifo majeruhi ajali ya Lori Moro kuongezeka yatajwa

DAKTARI Bingwa wa Upasuaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Edwin Mrema, amesema majeruhi wengi wa ajali ya moto wamepoteza maisha kwa sababu waliungua ndani ya mwili kwa asilimia 70 hadi 100.

Amesema wagonjwa hao waliathiriwa na moshi wa moto wa mafuta ya Petroli kuanzia kwenye mfumo wa upumuaji, mapafu, figo na mwili ukawa  wazi kwa asilimia 90 kutokana na majeraha ya moto na kusababisha ngozi nayo kupoteza kinga.

Daktari huyo anayetibu majeruhi hao wa moto, akizungumza na waandishi wa habari leo, amesema walipokelewa hospitalini hapo wakiwa na hali mbaya na siyo kwamba MNH haina wataalam na vifaa tiba.

Amesema kutokana na kuathirika ndani na nje ya mwili walilazimika kuwaweka mashine za kupumulia ili kuondoa hewa ya sumu waliyovuta aina ya 'Carbonmonoxide Poisoning' na kuwaingizia hewa safi ya Oxygen.