Sababu wanafunzi kufeli Hisabati zatajwa

22Jan 2022
Pastson Andugalile, TUDARCO
Dar es Salaam
Nipashe
Sababu wanafunzi kufeli Hisabati zatajwa

KAMISHNA wa Elimu, Dk. Lyabwene Mutahabwa, ametaja sababu za wanafunzi kufanya vibaya somo la Hisabati katika mitihani ya taifa ikiwamo mazingira ya ufundishaji kutokuwa rafiki na wezeshi.

KAMISHNA wa Elimu, Dk. Lyabwene Mutahabwa.

Sababu nyingine, amesema ni kutokuwapo kwa upendo kati ya mwanafunzi na mwalimu wa somo hilo, hali inayoweka uwoga wa kulielewa somo hilo.

Alibainisha hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa miongozo minne ya kufundishia elimu ya stadi za maisha kwa kuzingatia afya ya uzazi, Virusi vya Ukimwi (VVU), jinsia na kuhusiana kwa heshima kwa walimu wa shule za msingi na sekondari, iliyoandaliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

"Mlisikia juzi matokeo ya kidato cha nne katika somo la Hisabati yalikuwa si mazuri. Nimefuatilia katika baadhi ya shule nimekuta hivi, mwalimu akitoa hesabu 10 anakuwa na mzigo wa fimbo, mwanafunzi atakayekosa hesabu tano atachapwa viboko vitano, akikosa hesabu tatu atachapwa fimbo tatu.

Yaani unapigwa fimbo kulingana na idadi ya hesabu ulizokosa,” alisema. Dk. Mutahabwa alisema endapo kuna mwalimu mwenye dhana kwamba anapofundisha akitumia fimbo inasaidia kumjaza akili mwanafunzi, atakuwa anajidanganya na kwamba ualimu hauko hivyo.

Aliwashauri walimu wanaofundisha somo la Hisabati kuwa na ushirikiano, upendo na kuwa tayari wakati wote kuwasaidia wanafunzi.

Alisema kwa kufanya hivyo, wanafunzi wengi watafaulu somo hilo. Alibainisha kwamba utafiti umeonyesha kuwa ili mwanafunzi azingatie masomo ya mwalimu anayemfundisha, ni lazima kuwapo na upendo na heshima kati yao ili miaka ijayo mwanafunzi huyo atamani kuwa mwalimu.

“Utafiti umeonyesha kwamba ili mwanafunzi azingatie masomo yake la kwanza ni lazima akupende wewe unayemfundisha. Yaani uwe mfano wa kuigwa kwa wanafunzi, atamani unavyovaa, atamani unavyohusiana na wengine ofisini na jamii,” alisema.

Dk. Mutahabwa alisema endapo mwanafunzi atampenda mwalimu anayemfundisha, atalipenda pia somo husika analofundishwa na kulisoma mara kwa mara.

"Kipindi chako hatakikosa lakini ukiwa mwalimu uliyejaa matusi, ubabe, dharau, dhihaka, kashfa tu, vitisho na mzigo wa fimbo pembeni usitegemee kufanikiwa," alisema Dk. Mutahabwa.

Akizungumzia kuhusu miongozo hiyo, Dk. Mutahabwa alisema endapo mafunzo katika miongozo hiyo itapelekwa kwa walimu wote wa shule za msingi na sekondari italeta matokeo chanya katika ufundishaji.

Kadhalika alisema serikali itaendelea kushirikiana na wananchi na wadau katika kuboresha elimu nchini, kwani jitihada kubwa zimefanyika katika kujenga na kuboresha miundombinu ya elimu ikiwa ni pamoja na madarasa, kuongeza walimu, vitabu na samani.   

Habari Kubwa