Sababu ya kuripotiwa kesi za ukatili jinsia hii

09Dec 2016
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Sababu ya kuripotiwa kesi za ukatili jinsia hii

MRATIBU wa Chama Cha Waandishi wa Habari wanawake Tanzania (Tamwa) Zanzibar, Dk. Mzuri Issa, amesema kuripotiwa kwa wingi kesi za udhalilishaji kunatokana na kuwapo kwa nguvu nyingi katika utekelezaji wa shughuli za kupinga ukatili wa kijinsia.

Alisema masuala ya ukatili yamezungumziwa sana na kuonyesha athari zake katika ngazi ya familia, jamii na hata taifa, na elimu imetolewa kwa kiasi kikubwa na kusababisha kuwapo mwamko na kuyaripoti katika mamlaka husika kama polisi, hospitali na mahakama.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tamko la asasi za kiraia kuhusiana na kuchelewa kushughulikia kesi za udhalilishaji na ukatili wa kijinsia Zanzibar, Dk. Mzuri alisema kipindi cha mwaka 2014 hadi sasa jumla ya kesi 774 zimeripotiwa

. Alisema takwimu hizo ni kwa mujibu wa taarifa za polisi na kuwa kati ya kesi hizo, 140 (18%) ziko polisi wakati 127 (16%) ziko Ofisi ya Mwendesha Mashtaka na kesi tano zimetolewa hukumu.

“Najua watu watasema mbona wanaharakati wanajitahidi kushughulikia masuala haya, wakati bado kesi nyingi, lakini hili linafanyika kutokana na kuwa nguvu nyingi zmewekwa katika utekelezaji wa shughuli za kupinga ukatili wa kijinsia,” alisema.

Hata hivyo, alisema ni vyema kwa mahakama kutoa hukumu kubwa zitakazoweza kutoa fundisho kwa wengine hasa kifungo cha miaka 30 kutokana na kesi hizo kuathiri sana sekta ya elimu, maendeleo ya wanawake na watoto pamoja na nchi hupunguza juhudi za kupunguza umaskini na kuleta usawa wa kijinsia.

“Tukiendelea kutetea na kupinga ukatili wa kijinsia katika kuadhimisha siku 16 za kupinga udhalilishaji leo (jana) tunakutana na wawakilishi, madiwani, wawakilishi wa Jeshi la Polisi, mahakama, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka ili kujadiliana kuhusiana na ucheleweshaji wa kesi na utolewaji wa hukumu,” alisema.

Mkurugenzi wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC), Harusi Mpatani, alisema ushirikiano unahitajika ili kupambana na vitendo hivyo.

Ofisa kutoka Kituo cha Kulelea Watoto cha SOS, Juma Omar, alisema harakati za kupinga udhalilishaji wa kijinsia zinasaidia katika kulinda maisha ya watoto na wanawake wanaofikwa na matatizo hayo.

Tamko hilo limetolewa kwa pamoja na wanaharakati wa kutetea na kupinga ukatili wa kijinsia kupitia taasisi za Kituo Cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC),

Action Aid Tanzania, Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (Zafela), SOS, Zayedesa, Jumuiya ya Mtandao wa Kijinsia Zanzibar (ZGC), Tamwa Zanzibar na Save The Children.

Habari Kubwa