Sababu za bosi wa TIB kutumbuliwa

15Jul 2019
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Sababu za bosi wa TIB kutumbuliwa

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imesitisha uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TIB Corporate, Frank Nyabungege, kwa kile kilichoelezwa ni mwenendo usioridhisha wa benki hiyo.

ALIYEKUWA Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TIB Corporate, Frank Nyabungege.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na BoT, imebainisha kuwa uamuzi huo umesukumwa na mwenendo usioridhisha wa benki hiyo katika kuleta mabadiliko.

Aidha, kutokana na uamuzi huo, BoT kwa mamlaka iliyopewa na sheria ya benki na taasisi za fedha mwaka 2006 imemteua Fred Luvanda, kuwa

Kaimu Mkurugenzi.

Kabla ya uteuzi huo, Luvanda alikuwa Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha, na kwa nafasi ya sasa atasimamia shughuli zote za kiutendaji za benki ya TIB Corporate.

Taarifa hiyo ya Idara ya Uhusiano na Itifaki, ilieleza kuwa hatua hizo zimechukuliwa kwa lengo la kuboresha usimamizi na utendaji wa benki zinazomilikiwa na serikali.

“Benki Kuu ya Tanzania inauhakikishia umma kuwa benki ya TIB Corporate itaendelea kutoa huduma na madai yote yaliyoiva yatalipwa kama kawaida. Itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika benki ili kuhakikisha sekta ya fedha inakuwa stahimilivu,” alibainisha.