Sababu za NEC kutoongeza muda daftari wapigakura

18Jul 2019
Godfrey Mushi
MOSHI
Nipashe
Sababu za NEC kutoongeza muda daftari wapigakura

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema haitaongeza muda wa zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura ambalo limepangwa kisheria kufanyika kwa siku saba katika kila mkoa.

Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage.

Hayo yamo katika taarifa iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage, alipokuwa akizungumza na wanahabari mkoani Kilimanjaro kuhusu kukamilika kwa maandalizi ya uzinduzi wa zoezi hilo.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuzindua zoezi hilo leo katika Uwanja wa Mandela, Manispaa ya Moshi.

“Kwa mujibu wa Sheria za Uchaguzi kwa maana ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi na Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inao wajibu wa kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura mara mbili, kati ya uchaguzi ulioisha na tarehe ya uteuzi wa uchaguzi unaofuata,”alisema Jaji Kaijage

Jaji Kaijage alifafanua kuwa kabla hawajaingia katika zoezi hili, walifanya uandikishaji wa majaribio katika kata mbili, moja ikiwa ni ya Kihonda iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na Kata ya Kibuta iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe.

“Sasa katika siku hizi saba, tume ilijiridhisha kwamba zinatosheleza na kwa muda ambao tumepanga kuanzia saa 2:00 aubuhi hadi saa 10:00 jioni unajitosheleza. Kwa hiyo hatuna tashuwishi kwamba siku hizi saba zitatosheleza kabisa kwa maeneo yote na kama nilivyosema kwa kila kituo nchi nzima tutatumia siku saba,”alisisitiza.

Aidha, Mwenyekiti huyo wa NEC, alieleza kuwa kwa yule aliyekosa kwa bahati mbaya nafasi kwa sababu ni mgonjwa au amelazwa, ipo nafasi nyingine ya uboreshaji wa pili ambao utaanza pindi uboreshaji wa kwanza utakapokuwa umekamilika Machi mwaka 2020.

Katika uboreshaji huo, jumla ya vituo 37,407 vya kuandikisha wapigakura vitatumika kwa upande wa Tanzania Bara na vituo 407 kwa Zanzibar.

Pamoja na mambo mengine, Jaji Kaijage alitaja sababu sita zinazohusu uboreshaji wa daftrari la kudumu la wapigakura kuwa ni kuandikisha wapiga kura wapya waliotimiza umri wa miaka 18 ambao ni raia wa Tanzania kwa mujibu wa sheria.

Uboreshaji huo pia utahusu, kuandikisha wapigakura ambao watakuwa wametimiza umri wa miaka 18 ifikapo Oktoba 2020 na utahusu kuhamisha taarifa za wapiga kura waliohama kata au majimbo yao ya uchaguzi.

Aidha, uboreshaji huo utahusu kutoa kadi mpya kwa wapigakura waliopoteza kadi zao za kupigia kura zilizotolewa na tume mwaka 2015 au ambao kadi zao zimeharibika na kusahihisha taarifa za wapiga kura ambao taarifa zao zilikosewa wakati wa uandikishaji wa mwaka 2015.

Pia utahusu kuandikisha wale ambao wana sifa, lakini hawakujiandikisha mwaka 2015 na kufuta kutoka kwenye daftari taarifa za waliopoteza sifa kama vile waliofariki dunia.