Sababu za Sugu kurudi rumande

20Jan 2018
Grace Mwakalinga
Nipashe
Sababu za Sugu kurudi rumande

HAKIMU Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Michael Mteite, jana aliamuru Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi 'Sugu' na Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga,-

Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi 'Sugu' (Chadema) akipanda kwenye karandinga la polisi jana kurejea rumande ya Gereza la Ruanda mpaka keshokutwa baada ya kunyimwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya jana. PICHA: GRACE MWAKALINGA

Warudishwe rumande baada ya kutajwa kwa kesi yao ya kutumia lugha za fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.

Hakimu Mteite alisema sababu kuamuru washtakiwa hao kuendelea kubaki rumande kuwa kuwezesha kuharakisha usikilizwaji wa kesi, kutoa hukumu kwa wakati lakini pia kumpa nafasi Mbunge huyo kuendelea na majukumu mengine ya kibunge.

Sugu Masonga walipakiwa katika karandika la polisi baada ya uamuzi huo na kupelekwa mahabusu ya Gereza la Ruanda.

Sugu na Masonga wanakabiliwa na kesi ya kumdhalilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, John Magufuli, ambapo kwa mara ya kwanza walifikishwa mahakamani Jumanne.

Hakimu Mteite alisema kwa kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika kama ilivyodaiwa na wakili wa serikali, Joseph Pande, washitakiwa warudi mahabusu kwa ajili ya uharakishaji wa usikilizaji.

Mteite alisema endapo atatoa dhamana ipo hofu ya mshtakiwa kutohudhuria mahakamani hapo mara kwa mara wakati yeye anataka kesi hiyo iishe mapema.

Alisema amepanga kusikiliza kesi hiyo ndani ya wiki moja.

Pia alisema amewanyima dhamana washitakiwa kwa ajili ya usalama wao kwani wanaweza kudhuriwa na umma kwa tuhuma za kumchafua Rais ambaye kimsingi ni taasisi iliyochaguliwa na wananchi wote wa Tanzania, ikiwemo na Jimbo la Mbeya.

Washtakiwa hao wanadaiwa kufanya uchochezi kwa kutoa lugha ya fedheha dhidi ya Rais Magufuli Desemba 30, mwaka jana ambapo Sugu anadaiwa kutamka kuwa Rais ni muuaji. 

Habari Kubwa