Sabaya akana kutakatisha fedha

22Jan 2022
Allan Isack
Arusha
Nipashe
Sabaya akana kutakatisha fedha

ALIYEKUWA Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya, amedai kuwa hakuwahi kutakatisha Sh. milioni 90 wala kutoa mgawo wa fedha kwa vijana wanaodaiwa kuwa ni wake.

Sabaya ambaye ni shahidi wa pili na mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya uhujumu uchumi namba 27 na wenzake sita, alitoa madai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Patricia Kisinda, anayesikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mkoa wa Arusha.

Mbali na Sabaya, washtakiwa wengine ni Sylvester Nyegu (26), Enock Togolani (41), Watson Mwahomange (27), John Odemba, Jackson Macha (29) na Nathan Msuya (31). 

Akiongozwa na Wakili wa Utetezi, Fridolin Bwemelo, Sabaya alidai kwamba hakuwahi kutoa mgawo wa fedha kwa vijana wanaodaiwa kuwa ni wake kwa kuwa hawafahamu kabisa.

"Mheshimiwa hakimu mimi sijatakatisha fedha wala kutoa mgawo kwa mtu yeyote ambaye simfahamu na eneo wanalodai kwamba nilifanya mgawo huo siku hiyo, sikuwapo. Nilikuwa Hai, Kilimanjaro," alidai Sabaya.

Pia alikana kutakatisha Sh. milioni 90 na hakukuwa na sababu kwa upande wa mashtaka kupeleka gari lake mahakamani kama kielelezo cha ushahidi kwa kuwa halihusiani na hati ya mashtaka kwa kuwa alilinunua kwa Sh. milioni 60. 

"Gari langu VX V8 T222DBY sikulinunua Januari 22, 2021 lakini limeletwa mahakamani kama kielelezo cha ushahidi ilihali halihusiki katika hati ya mashtaka.

"Mheshimiwa hakimu mashtaka ya kugawa fedha kwa kutakatisha dhidi yangu si ya kweli. Hati ya mashtaka ni batili kwa kuwa hapa mahakamani sina shtaka la kutakatisha fedha nikiwa Dar es Salaam au hoteli ya Tulia Lodge, hivyo shtaka hili ni la uongo kwa kuwa wameshindwa kuthibitisha,” alidai.

Sabaya pia alikana kumtuma Mwahomange  anayedaiwa kuwa alimwagiza kupeleka pampu kutengenezwa katika Karakana ya mfanyabiashara Francis Mroso.

"Shahidi wa nne wa mashtaka Philemon Kazibira, ambaye ni karani wa Mroso, alidai kwamba aliniona mimi nikiwa nimeambatana na vijana wanne na baada ya hapo niliagiza mfanyabiashara huyo kuitwa kufika ofisini hapo.

"Invoice na ripori, inayodaiwa na  shahidi wa nne baada ya pampu kutengenezwa havijawahi kuletwa hapa mahakamani kama uthibitisho kama kuna pampu ilikwenda kutengezwa katika Karakana hiyo. Hakuna kitu kinachothibitisha kwamba pampu ilipelekwa katika eneo hilo,” alidai Sabaya.

Akiongozwa na wakili mwingine wa utetezi, Sylvester Kahunduka, Sabaya alidai kwamba maofisa wa TAKUKURU, hawakufuata sheria na pia hawakuwa na kibali cha kusachi.

Sabaya alidai kuna vitu ambavyo vimekamatwa na maofisa wa TAKUKURU na polisi lakini wameficha taarifa zake, hawataki kuziweka wazi.

"Wamechukua vitu bila ya kutoa kibali cha kukamata, pia baadhi ya vitu walivyokamata hawataki kutoa taarifa zake na kuziweka wazi. Wanadai kwamba wakati walipotuvamia na kutukamata walitukuta na simu kama ni kweli tulikuwa nazo wangeonyesha ni simu ngapi, alidai.

Pia alidai kwamba hakuna shahidi yeyote wa mashtaka aliyefika mahakamani na kudai alishuhudia na kuona akikabidhiwa Sh.milioni 90.

Habari Kubwa