Safari Bunge la 12 rasmi

08Nov 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe Jumapili
Safari Bunge la 12 rasmi

MKUTANO wa kwanza wa Bunge la 12, unatarajiwa kuanza Novemba 10 mwaka huu huku majukumu sita yakitajwa kufanyika ndani ya siku nne tu ikiwamo uchaguzi wa spika na kuthibitisha jina la Waziri Mkuu.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini hapa, Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai, alisema kikao hicho kimeitishwa baada ya Tangazo la Rais lililotolewa Novemba 5 mwaka huu kwenye Gazeti la Serikali toleo maalum namba 942A.

Pia, alisema utaratibu huo unafuatia tangazo alilolitoa kwenye gazeti hilo hilo toleo maalum namba 1763A na 1764A Novemba 5, mwaka huu kuhusu kuwa wazi kwa nafasi ya spika na naibu spika pamoja na kanuni za uchaguzi wa viongozi hao.

“Wabunge wote wanafahamishwa kwamba shughuli za usajili na taratibu zingine za kiutawala zitafanyika Ofisi ya Bunge Dodoma kuanzia tarehe 7-9, Novemba mwaka huu, hivyo kikao cha kwanza cha mkutano wa kwanza wa Bunge kitafanyika Novemba 10, mwaka huu kama ilivyotamkwa kwenye Tangazo la Rais," alisema.

Alitaja shughuli zitakazofanyika kuwa ni kusomwa kwa tangazo la Rais kuitisha Bunge, uchaguzi wa spika, kiapo cha uaminifu kwa wabunge wote, kuthibitisha jina la Waziri Mkuu, uchaguzi wa naibu spika na ufunguzi rasmi wa bunge jipya utakaofanywa na Rais Dk. John Magufuli.

Vilevile, aliwasisitiza wabunge wateule wote kufika wakiwa na nyaraka mbalimbali ikiwamo hati ya kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa mbunge, nakala ya kitambulisho cha taifa, kadi ya benki yenye namba ya akaunti ya mbunge na cheti cha ndoa kinachotambuliwa na serikali kwa wenye ndoa.

“Nyaraka zingine ni cheti cha kuzaliwa cha watoto wenye umri chini ya miaka 18 kwa wenye watoto, vyeti vya elimu au taaluma, picha nakala nane na nakala ya wasifu wa mbunge," alisema.

Alifafanua kuwa nakala ya wasifu wa mbunge ni muhimu kwa kuwa wanaitumia wakati wa kupanga wajumbe wa kamati za kudumu za Bunge.

Alipoulizwa kuhusu kuhitimishwa kwa Bunge, katibu huyo alisema shughuli hizo zinatarajiwa kuhitimishwa Ijumaa Novemba 13, mwaka huu.

Uzoefu unaonyesha mkutano huo wa kwanza wa Bunge umekuwa ukifanyika kwa wiki mbili, lakini safari hii muda unaonekana kupunguzwa.

Habari Kubwa