Sakata la makinikia lafufuliwa bungeni

28May 2019
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe
Sakata la makinikia lafufuliwa bungeni
  • *Upinzani wahoji ziliko tril. 424/- za Acacia na tril. 1.6/- za Barrick

KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni imelifufua sakata la makinikia, ikitaka kujua sababu za kutolipwa kwa Dola za Marekani milioni 700 (Sh. trilioni 1.604) ambazo serikali ilisema itapewa na Kampuni ya Barrick.

John Heche.

Akiwasilisha hotuba yake bungeni jijini Dodoma jana kuhusu makadirio ya bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka ujao wa fedha, Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Madini, John Heche, alisema makubaliano hayo ya serikali na Barrick bado hayajatekelezwa huku Acacia, kampuni tanzu ya Barrick wakiendelea kuchimba dhahabu nchini.

Heche alisema Machi 2, 2017, Wizara ya Nishati na Madini ilitoa taarifa kwa umma kuwajulisha wafanyabiashara na kampuni zinazojihusisha na shughuli za uvunaji wa madini, kuacha mara moja shughuli za usafirishaji wa makinikia na mawe yenye madini ya metaliki kama vile dhahabu, shaba, nikeli na fedha.

Aliongeza kuwa mbali na katazo hilo, Rais aliunda kamati mbili za uchunguzi wa usafirishaji wa makinikia nje ya nchi na kwamba pamoja na mambo mengine, ripoti zote zilizungumzia hasara kubwa inayopata Tanzania kutokana na sheria mbovu za madini na mikataba iliyoingiwa na serikali na wawekezaji.

Alisema ripoti zote mbili zilijikita katika kubaini viwango vya madini vilivyoko katika makinikia na mikataba ya uchenjuaji ambayo haikuwa wazi.

"Ripoti ya makinikia ya Mgodi wa Bulyanhulu na Buzwagi inaonyesha kuwa Kampuni ya Acacia ambayo ndiyo mmiliki wa migodi hiyo, ilikuwa inadaiwa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), kiasi cha Dola za Marekani bilioni 190 (Sh. trilioni 424) ambayo ni kodi iliyokuwa ikikwepwa pamoja na riba," alisema.

Heche aliongeza: "Kiasi hiki cha fedha kiliwafanya Watanzania kuwa na matumaini makubwa, wengi wao wakiamini kila Mtanzania ataweza kumiliki gari aina ya Noah na wengine wakiamini huduma za kijamii zitapatikana bure.

"Hata hivyo, Acacia waliikataa taarifa iliyotolewa na serikali kuwa haijawahi kukwepa kodi na huilipa serikali asilimia nne ya mirabaha ya dhahabu, shaba na fedha kwenye makinikia kama ilivyo katika makubaliano baina yake na serikali.

"Tutakumbuka mwaka 2007, kampuni hii ilituhumiwa kukwepa kodi na kuzua mtafaruku mkubwa na serikali ya wakati huo.

"Katika makubalino, Barrick iliahidi kulipa Dola milioni 700 wakati mazungumzo zaidi yakiendelea ili kuona namna gani nchi itanufaika, lakini hadi sasa, fedha hizo hazijatolewa, huku Acacia wakiendelea kuchimba dhahabu katika migodi wanayoimiliki nchini.

"Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kufahamu kwanini fedha hizo hazijalipwa hadi sasa? Ikiwa kweli Acacia walipaswa kulipa malimbikizo ya kodi na tozo na hadi sasa hawajalipa, kwanini wanaendelea na shughuli za uchimbaji madini nchini wakati tuliambiwa ni wezi wa rasilimali za nchi yetu?"

Katika hotuba yake hiyo, Heche pia alisema kambi hiyo inataka kujua sababu za serikali kutoa fedha ambazo hazifiki hata asilimia moja ya fedha za maendeleo.

Alibainisha kuwa wizara hiyo katika mwaka huu wa fedha, iliidhinishiwa na Bunge Sh. bilioni 19.62 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Hata hivyo, hadi kufikia Februari mwaka huu, wizara hiyo ilikuwa imepokea Sh. milioni 100, sawa na asilimia 0.5 ya bajeti iliyoidhinishwa.

BILIONI 100/-Heche pia alisema kambi yao inaitaka serikali kuacha mazoea ya kuvunja sheria za nchi ambazo viongozi wamekula viapo kuzilinda.

Alisema kambi imebaini taarifa za wizara hiyo katika mwaka huu wa fedha zinaonyesha imepokea Sh. bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya wizara eneo la Ihumwa, jijini Dodoma.

"Pamoja na malengo mazuri ya ujenzi wa ofisi, Kambi Rasmi ya Upinzani tunaona siyo sawa Wizara ya Fedha na serikali kutoa fedha ambazo hazikuwa kwenye bajeti.

"Ikiwa serikali ilikusudia kujenga ofisi hiyo, kwanini haikuomba bajeti yake ndani ya Bunge hili ili kuidhinishiwa na Bunge hili?

"Na ikiwa serikali ilipata wazo hili baadaye, kwanini haikufuata utaratibu wa kisheria ya bajeti ya nyongeza kwa matakwa ya sheria za nchi?" Heche alihoji.

Waziri kivuli huyo pia alisema kambi yao inataka kujua lini urasimu unakwamisha mradi wa chuma wa Mchuchuma na Liganga zitakwisha ikiwa ni pamoja na kuangalia masharti mapya ya uwekezaji chini ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2017.

Heche pia alisema kambi inaishauri serikali kuhakikisha sheria zinazohusu rasilimali za nchi kama sekta ya madini, mafuta na gesi asilia zipitiwe upya ili kumpa mamlaka ya moja kwa moja Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kupata taarifa zitakazosaidia ukaguzi wake kwa maslahi mapana ya nchi.

Mbunge huyo wa Tarime Vijijini (Chadema) pia aliitaka serikali kulieleza Bunge kiasi ambacho wananchi wanaozunguka Mgodi wa Nyamongo, North Mara, watalipwa kama fidia kutokana na madhara waliyopata kufuatia mgodi huo kutitirisha maji machafu yenye sumu kwenye makazi ya watu.

Alisema tayari serikali imeipiga faini ya Sh. bilioni 5.6 Kampuni ya Acacia kama adhabu kwa kushindwa kudhibiti bwawa la maji yenye sumu na kuhatarisha afya za wakazi wanaozunguka mgodi huo.

Habari Kubwa