Sakata jiwe la rubi latikisa Bunge

22Apr 2022
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Sakata jiwe la rubi latikisa Bunge

MJADALA umeibuka bungeni na mitandao ya kijamii baada ya jiwe lenye madini aina ya rubi lenye uzito wa kilo 2.8 kuonekana katika maonyesho jijini Dubai, huku likidaiwa limetoka Tanzania.

Jiwe hilo lenye thamani ya Dola za Marekani milioni 120 (Sh. bilioni 240) limeibua  gumzo baada ya kutofahamika limepita njia gani hadui kufika Dubai, huku serikali ikikiri kupata taarifa za uwapo wa jiwe hilo, kuanza kukusanya taarifa za kiuchunguzi na kuahidi kuzitolea ufafanuzi bungeni.

Akitoa ufafanuzi bungeni jana, Naibu Waziri wa Madini, Dk. Stephen Kiruswa, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mkinga (CCM), Dunstan Kitandula, alisema taarifa za awali zinaonesha kuwa mmiliki wa sasa wa jiwe hilo anaishi Marekani katika Jimbo la California na tayari serikali imeanza kuwasiliana naye tangu juzi.

Katika swali lake, Kitandula aliuliza: “Jiwe la rubi lenye uzito wa kilo 2.8 lipo kwenye maonyesho kwa sasa jijini Dubai na linasadikika kutoka Tanzania na siku chache zijazo kutakuwa na mnada wa kuuza jiwe hilo. Je, nchi itanufaika vipi na mnada huo?”

Akijibu swali hilo, Dk. Kiruswa alisema Aprili 13, mwaka huu, Wizara ya Madini ilipata taarifa kupitia mitandao ya kijamii kwamba kuna jiwe ambalo limepewa jina Akbar Alhamal ambalo linakwenda kuwekwa mnadani ndani ya siku 30 baada ya mfungo wa Ramadhan na kudaiwa limetoka Tanzania.

“Mheshimiwa Spika, mara baada ya kupata habari hizo, wizara imechukua hatua za haraka kutafuta kama habari hizo ni za kweli. Kwa kuwa jiwe limeshavuka mipaka ya Tanzania, tunaendelea kukusanya taarifa ili kuzitoa katika bunge lako tukufu, zinahusisha nchi ya Dubai na tayari ubalozi wa Tanzania na wizara zinawasiliana kufuatilia ukweli na uhalisia wa bei,”alisema.

Dk. Kiruswa alisema kutokana na mmiliki wa sasa wa jiwe hilo kuwa yuko Marekani, wigo wa kidiplomasia umepanuka kutokana na kuhusisha nchi tatu.

“Nikuhakikishie Mheshimiwa Spika kwamba tutakapokuwa tumepata nyaraka za usafirishaji wa jiwe hili kama kweli limetoka Tanzania, tutapata nyaraka za thamani na asili ya hili jiwe limetoka wapi, tukipata na nyaraka za mauziano za mmiliki wa sasa na wa awali, tutatoa taarifa katika bunge lako kama lipo na kama ni la kwetu, tuwahakikishie Watanzania haki yao haitapotea na sheria, kanuni na taratibu zitahakikisha rasilimali hii inatumika kwa manufaa ya nchi yetu,” alisema.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Rorya (CCM), Jafari Chege, alihoji ni lini uchimbaji wa madini ya dhahabu utaanza katika eneo la Utegi katika Tarafa ya Girango.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri huyo alisema Wizara ya Madini imeendelea kutoa leseni za utafutaji wa Madini nchini.

“Katika eneo la Utegi kuna leseni za utafutaji wa madini za Kampuni ya North Mara Gold Mine Limited na ABG Exploration Limited. Kwa sasa kampuni hizi zinaendelea na utafutaji wa madini katika eneo hilo,” alisema.

Pia alisema uchimbaji wa madini hutegemea kukamilika kwa mafanikio kwa  utafutaji wa madini ambao huhusisha shughuli za kijiolojia.

“Aidha, shughuli hizi huchukua gharama kubwa na muda mrefu. Kwa msingi huo, eneo la Utegi linatarajiwa kuanza uchimbaji baada ya utafiti kukamilika na kuonekana kwa mashapo yenye kutosheleza kuanzisha uchimbaji kwa faida,”alisema.

Pia alisema serikali kupitia Tume ya Madini inafuatilia kwa karibu shughuli za utafutaji wa madini zinazofanyika nchi nzima.

Habari Kubwa