Sakata kina Mdee bado kizungumkuti  

14May 2022
Na Waandishi Wetu
DAR ES SALAAM, DODOMA
Nipashe
Sakata kina Mdee bado kizungumkuti  

HATIMA ya wabunge 19 wa viti maalum waliovuliwa uanachama na vikao vya juu vya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) bado ni kizungumkuti kutokana na uongozi wa Bunge kutochukua hatua dhidi yao.

Halima mdee.

Baadhi ya wabunge hao ambao Baraza Kuu la CHADEMA lilitangaza usiku wa kuamkia juzi kuunga mkono uamuzi wa Kamati Kuu wa kuwavua uanachama, jana walihudhuria kikao cha Bunge la Bajeti jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema, alipoulizwa na Nipashe kuhusu barua yao kwa uongozi wa Bunge dhidi ya wabunge hao, alidai tayari imeshafika rasmi mezani kwa Spika.

Alidai kuwa waliwasilisha barua hiyo kwa Spika jana asubuhi kumjulisha kuhusu uamuzi wa Baraza Kuu kuwa limeridhia wabunge hao 19 kufutwa uanachama wa CHADEMA.

"Kwa hiyo, ni wajibu wa Spika kuchukua hatua, wao kwenda bungeni siyo tatizo kwa sababu bado Spika hajachukua hatua, tunasubiri Spika atoe kauli," alisema.

 

KUTAMBUA UCHAGUZI

Alipoulizwa na Nipashe kama CHADEMA itapeleka majina mapya ya wabunge wa viti maalum ilhali ilishatangaza haikutambua Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, Mrema alisema mpaka sasa suala hilo halijazungumzwa na litategemea hatua ambazo Spika atazichukua dhidi ya wabunge hao 19 wanaoongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA).

"Kamati Kuu ikiamua kuteua au isipoteua ni wajibu wake. Kwa sasa hakuna kauli kwa sababu Kamati Kuu haijakaa na kujadili jambo hili," alisema.

 

WATINGA BUNGENI

Licha ya uamuzi wa kuvuliwa uanachama ulioridhiwa na Baraza Kuu juzi, baadhi ya wabunge hao jana waliingia bungeni majira ya  saa tatu asubuhi na kushiriki kikao cha chombo hicho.

Wabunge ambao Nipashe iliwashuhudia bungeni jana kutoka kundi hilo la wabunge 19 waliofutwa uanachama: Salome Makamba, Esther Matiko, Tunza Malapo, Jesca Kishoa, Anatropia Theonest, Asya Mohamed, Stella Fiao.

Wakiwa kwenye shughuli za Bunge kipindi cha 'Maswali', baadhi ya wabunge hao walipewa nafasi ya kuuliza maswali ambayo yalijibiwa na mawaziri husika. Waliopata nafasi ya kuuliza swali ni Salome, Tunza na Asya.

 

MWENYEKITI  MAADILI

Nipashe ilizungumza na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge, Emmanuel Mwakasaka, kwa lengo la kupata maoni kuhusu kurejea kwa wabunge hao bungeni licha ya kufutwa uanachama wa CHADEMA.

Mwakasaka alisema: “Msemaji Mkuu wa suala hilo ni Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackon, yeye ndiye atatuambia kama mkuu wa mhimili huu kuna nini kinaendelea.

“Kwa sababu yale yaliyotokea CHADEMA hayaingii moja kwa moja kwenye Bunge, sisi hatufahamu kama Spika ameshapokea taarifa."

Mwakasaka ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini, alisema amewaona bungeni wabunge hao na bado anawatambua kuwa ni wabunge.

"Wenzetu tumewaona leo (jana) bungeni na bado tunawatambua kama wabunge wenzetu, ndiyo maana leo wapo bungeni. Sasa katika hatua hii sisi tunasubiri taarifa ya mkuu wetu wa mhimili atatueleza nini. Lakini haya matangazo mengine tunaendelea kuyasubiri kutoka kwa Spika,” alisema Mwakasaka.

Alisema kama kuna barua imeandikwa, itapelekwa kwa mhusika ambaye ni Spika wa Bunge au Katibu wa Bunge, akifafanua: "Kuna wakati barua wanaielekezea kwa Spika wa Bunge mwenyewe, sasa ikishafika nini kinakuja baada ya hapo? Spika mwenyewe atatujulisha sisi wenyeviti wa kamati, lakini hadi sasa tunavyozungumza na ninyi hatujapokea taarifa yoyote kutoka kwa Spika."

KATIBA INASEMAJE?

Kifungu cha 1(e) cha Ibara ya 71 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, kinaelekeza hatua za kuchukuliwa dhidi ya mbunge aliyepoteza uanachama wa chama cha siasa.

Inatamkwa katika kifungu hicho kuwa: "Mbunge atakoma kuwa mbunge na ataacha kiti chake katika Bunge ikiwa mbunge huyo ataacha kuwa mwanachama wa chama alichokuwamo wakati alipochaguliwa au alipoteuliwa kuwa mbunge."

*Imeandikwa na Gwamaka Alipipi (DODOMA na Romana Mallya (DAR)

Habari Kubwa