Sakata la kikokotoo maumivu mafao sekta binafsi 

11Jan 2019
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Sakata la kikokotoo maumivu mafao sekta binafsi 

BAADA ya serikali kutoa maelekezo ya kurejea katika kikokotoo cha zamani, wastaafu wanaotoka sekta binafsi sasa wataendelea kulipwa mafao ya mkupuo kwa asilimia 25 ya michango yao, huku wale wa sekta ya umma wakilipwa kwa asilimia 50.

Kanuni za Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ya Mwaka 2018, ziliweka kikokotoo kimoja cha asilimia 25 ambacho kiliweka usawa kwa wastaafu wote kupata mafao yenye fomula moja, tofauti na awali kulipokuwa na fomula mbili.

Kikokotoo kipya kwenye kanuni kilikuwa ni asilimia 25 kwa mafao ya mkupuo na asilimia 75 inayobaki kulipwa kama pensheni ya mwezi kwa kila mwezi hadi mwanachama atakapofariki dunia.

Hata hivyo, katika kikokotoo hicho, umri wa kuishi umekadiriwa kuwa ni miaka 12.5, ikiwa ni umri uliokadiriwa kuwa mwanachama ataishi baada ya kustaafu.


Kutokana na agizo la Rais John Magufuli la kurudi kwenye kikokotoo cha zamani, sasa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), ambalo linahudumia wanachama wa sekta binafsi na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ambao unahudumiwa wanachama ambao ni wafanyakazi wa serikali, watakuwa na fomula tofauti katika ulipaji wa mafao.

Kwa mujibu wa kikokotoo cha NSSF ambacho kimekuwapo kwenye kanuni za shirika hilo tangu mwaka 2014, mwanachama anapostaafu analipwa asilimia 25 ya mafao ya mkupuo na kilichobaki kinalipwa kama mshahara wa kila mwezi.


Kwa kanuni za PSPF na LAPF, ambazo sasa zitatumiwa na PSSSF ambayo imejumuisha mifuko ya GEPF, LAPF na PSPF, itatumia kanuni ambayo mwanachama analipwa asilimia 50 kwa mkupuo na kuendelea kulipwa kila mwezi kama mshahara kwa asilimia 50 iliyobakia.

Kikokotoo cha NSSF kwa pensheni nzima ni moja ya 580 mara jumla ya mishahara mara mishahara minono ya miaka mitatu kwa kipindi cha miaka 10 ya mwisho mara mishahara minono.

Kikokotoo cha malipo ya mkupuo ni moja ya 580 mara jumla ya mishahara mara mishahara minono mitatu ya miaka 10 ya mwisho mara 12.5 mara asilimia 25.
Kwa upande wa pensheni ya mwezi, ni moja ya 580 mara jumla ya mishahara mara mishahara minono mitatu ya miaka 10 ya mwisho mara asilimia 75 mara 1/12.

Kikokotoo cha PSSSF kwa sasa pensheni nzima ni moja ya 540 mara jumla ya mishahara mara mishahara minono mitatu ya miaka 10 ya mwisho.

Kwa malipo ya mkupuo ni moja ya 540 mara jumla ya mishahara mara mishahara minono ya miaka mitatu ya miaka 10 ya mwisho mara 15.5 mara asilimia 50.

Kwa upande wa pensheni ya mwezi, ni moja ya 540 mara jumla ya mishahara minono mitatu ya miaka 10 ya mwisho mara asilimia 50 mara 1/12.

Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ya Mwaka 2018, imetaja jumla ya mafao saba ambayo ni manne ya muda mfupi (fao la upotevu wa ajira, fao la ugonjwa, fao la uzazi na mkopo wa nyumba) na matatu ya muda mrefu ambayo ni pensheni ya uzeeni, fao la ulemavu na fao la warithi.

Habari Kubwa