Salamu  za Mwinyi viongozi wa dini

17Apr 2018
Salome Kitomari
DAR ES SALAAM
Nipashe
Salamu  za Mwinyi viongozi wa dini

RAIS mstaafu Ali Hassan Mwinyi jana aliwataka viongozi wa dini nchini kuhubiri amani bila kuangalia madhehebu, itikadi na historia bali uhai wa mwanadamu.

RAIS mstaafu Ali Hassan Mwinyi.

Akizungumza jana wakati wa mkutano wa kamati ya amani ya mkoa wa Dar es Salaam, Mwinyi aliyeongoza nchi kati ya 1985-1995 alisema dini zote zimetaja neno amani kwenye vitabu vyake na hivyo kila mmoja anapaswa kuihubiri bila kuchoka kwa kuwa ndiyo uhai wa binadamu.

Kauli ya Mwinyi inafanana na nasaha za Rais John Magufuli kwa viongozi wa dini Jumapili mbili zilizopita ambapo aliwataka kushirikiana na serikali yake ili kuendeleza amani iliyoachwa na waasisi.

Rais Magufuli alikuwa akizungumza Aprili 8 wakati wa sherehe za kumsimika Askofu Mkuu Isaac Amani wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha.

Aliwaomba viongozi wa dini kuendelea kuiombea serikali yake na viongozi wote ili kuendeleza mshikamano na amani ambayo ni tunu ya taifa.

Aidha, Rais Magufuli alisoma mistari kadhaa ya Bibilia yenye kusisitiza amani na kuomba kila mmoja nchini aendeleze amani hiyo.

Akizungumza jana jijini, Mwinyi maarufu Mzee Ruksa alisema: "Hii kamati haitaki maneno mengi, ina kazi kubwa na muhimu kwa jamii na maamuzi yenu (viongozi wa dini) isogee imfikie kila mtu bila kujali dini yake, hadhi, kwa uhai, furaha na kwa ajili ya maisha ya mwanadamu."

Mwinyi alisema neno amani linaonekana dogo lakini limebeba ujumbe mzito katika mahusiano, maisha na kazi kwa wanajamii.

"Neno amani linatajwa sana kwenye mazungumzo, lipo kwenye fikra zetu, linasomeka kwenye vyombo vya habari, mikutano ya kitaifa na kimataifa. Amani ni uhai kwa nchi na wananchi pasipo amani hata uwezo wa kufikiri haupo," alisema.

Mwinyi alisema amani inaweza kuonekana ni neno la kawiada, lakini katika Qurran Mungu anasema amani ni neno linalotoka na kuwa mwenye huruma na huruma ni utu, huku kwenye Ukristo injili imezungumzia amani ikiwataka watu kutafuta amani kwa watu wote.

"Tanzania kama sehemu ya jamii ya kimataifa inayoishi katika uhalisia wa kuwapo kwa dini mbalimbali, kwa miaka mingi imejulikana na inajulikana kama kisiwa cha amani," alisema.

"Wananchi wanaishi kwa pamoja, ushirikiano, utulivu na mshikamano bila kujali dini, kuwa na tofauti za kabila, historia, kisiasa, na dini yenyewe, lazima ilindwe kwa nguvu zote." 

Rais huyo mstaafu alisema yote yamewezekana kwa sababu ya amani ambayo viongozi wa dini wameifundisha na waendelee kuilea jamii na kuiweka katika mzunguko mzima wa maisha ya uaminifu.

"Tanzania kama sehemu ya jamii ya kimataifa tunaishi katika uhalisia wa uwepo wa dini mbalimbali, hivyo lazima tushiriki kuilinda amani," alisema.

Alipozungumza hadharani Oktoba 13, 2016, Mwinyi alisema nchi inakabiliwa na changamoto ya ubaguzi wa dini na ukabila pamoja na mmomonyoko wa maadili.

Alisema katika kipindi cha miaka 17 ya kutokuwapo kwa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mpaka siku hiyo, wanasiasa wamekuwa wakitumia majukwaa kueneza dini na nyumba za ibada kueneza siasa, hali ambayo alibainisha kuwa inasababisha mmomonyoko wa maadili.

Mwinyi aliyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akifungua kongamano la Kumbukumbu ya Miaka 17 ya Mwalimu Nyerere lililoandaliwa na Taasisi ya Uongozi kwa kushirikiana na ubalozi wa China nchini.

Kongamano hilo lililokuwa na ujumbe wa "Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere: Mafundisho kwa viongozi wa sasa na kizazi cha baadae", pia lilifanyika sanjari na uzinduzi wa kitabu kinachoelezea maisha ya Mwalimu Nyerere kilichoandaliwa na watu wa China kwa ajili ya kujifunza mambo aliyoyafanya.

Kitabu hicho kimeandikwa kwa lugha ya Kichina ili raia wa nchi hiyo wajifunze maisha ya Mwalimu Nyerere.

Mwinyi alifafanua kuwa kama nchi itakubali kuwa changamoto ya ubaguzi wa kidini na ukabila upo, itakuwa ni ishara ya kurudi kwenye mstari na misingi aliyoiacha Mwalimu Nyerere.

Habari Kubwa