Salamu mpya za bomoabomoa 

17Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Salamu mpya za bomoabomoa 

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Kilimanjaro, Daudi Mrindoko amewataka watu waliovamia maeneo ya shule zinazomilikiwa nayo na kujenga makazi ya kudumu kuhama kwa hiari badala ya kusubiri kuvunjwa.

Mrindoko alitoa tahadhari hiyo jana baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika Shule ya Sekondari Kibo iliyopo Manispaa ya Moshi na kukutana na wajumbe wa bodi wa shule hiyo.

Akiwa shuleni hapo, alieleza kushangazwa kwake na ujenzi wa makazi unaoendelea kufanywa na baadhi ya wananchi ambao wamevamia eneo la shule.

“Wapo baadhi ya watu wamevamia maeneo ya shule zetu na kujenga makazi, lakini niwaagize waanze kuondoa wenyewe makazi yao kabla ya sheria kuchukuliwa," alisema Mrindoko. "Kibo ilikuwa na eneo la ekari 20 lakini sasa hivi imebakiwa na ekari 15 tu.”

Alisema ingawa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk. John Magufuli ameunda tume ya kuchunguza mali za chama, yeye ameanza kushughulika nao kwanza kabla tume hiyo haijafika Kilimanjaro.

Mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa katika kipindi chake cha miaka mitano ya uongozi wa jumuiya hiyo atahakikisha miradi yote inakuwa salama. 

Habari Kubwa