Samaki chanzo kutumbuliwa afisa uvuvi

07Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Samaki chanzo kutumbuliwa afisa uvuvi

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amemuagiza  Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dk. Yohana  Budeba kumsimamisha  kazi Afisa Kitengo cha Doria na Udhibiti wa Uvuvi Mkoa wa Kagera, Ayoub Ngoma kwa tuhuma za  kushiriki  katika utoroshaji wa samaki wenye uzito wa tani 2.5 kwenda nchini Burundi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina

Mpina  amesema Disemba 3, mwaka huu majira ya Saa 3:00  asubuhi, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ngara ilikamata gari lenye namba za usajili T 614 CLQ aina ya Mitsubishi Canter likiwa limepakia Samaki wenye uzito wa tani 2 aina ya Sangara na kilo 530 aina ya Sato kwenye mpaka wa Murusagamba wilayani Ngara wakiwa na thamani ya Sh. milioni 20.8.

“Katika kipindi cha uongozi wangu, tayari nimesha waagiza Makatibu Wakuu waliopo katika Wizara yangu kutembea na  barua zilizozosainiwa za kusimamisha kazi watumishi wote wanaohujumu jitihada za Serikali ibaki kujaza jina tu. Kwa sasa hatuna hata nusu dakika ya uvumilivu kwa watu kama hawa, tutawaondoa mara moja,” Amesema Mpina

Waziri Mpina amesema Afisa huyo na Dereva wa gari hilo, Ayuob Sanga wanashikiliwa na polisi kwa hatua za kisheria kwa kuhusika na tukio hilo,  na kuongeza kwamba samaki hawa walikuwa wakitoroshwa kwenda nje ya nchi bila ya kufuata Sheria ya Uvuvi Na 22 ya 2003 na taratibu mbalimbali za usafirishaji wa samaki na mazao yake nje ya nchi.

Habari Kubwa