Samaki waliokufa wazagaa ufukweni

22Jul 2021
Romana Mallya
DAR ES SAALAM
Nipashe
Samaki waliokufa wazagaa ufukweni

SAMAKI waliokufa wameonekana kwenye ufukwe wa Bahari ya Hindi eneo la Aga Khan jijini Dar es Salaam.

Mamlaka za serikali zimekiri kuonekana kwa samaki hao na tayari uchunguzi umeanza kubaini chanzo chake.

Mmoja wa mashuhuda aliyekuwa sehemu ya timu ya maofisa wa serikali waliozuru eneo la tukio jana, aliliambia Nipashe kuwa suala hilo lipo kwenye uchunguzi wa Jeshi la Polisi na mamlaka zingine za serikali na tayari sampuli zimechukuliwa kwenda kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.

Ofisa huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa kuwa si msemaji, alisema samaki hao walionekana kwenye eneo hilo Aga Khan.

“Tulijaribu kukusanya na zilifika kilo zaidi ya 150, ila kwa sasa ni mapema kulizungumzia suala hili,” alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk. Samuel Gwamaka, alipoulizwa kuhusiana na samaki hao, alisema kwa wakati huo hakuwa na taarifa na kuahidi kutuma wataalamu wake kwenda eneo la tukio.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Dk. Ismail Kimirei, alikiri samaki hao walionekana eneo hilo la ufukwe lakini polisi waliingia kati mwanzoni na waliwapa taarifa maofisa wa Wizara ya Mifugo ambao mara moja walikwenda eneo la tukio.

“Tukafika na watu wa wizara tumechukua sampuli na zingine zimekwenda maabara ya taifa ya wizara na polisi kwa ajili ya kupeleka kwa Mkemia Mkuu, tunasubiri majibu.

"Samaki waliokusanywa walikuwa ni wa aina mbalimbali lakini wengi wao ni watoto na ziliokotwa kilo 160,” alisema.

Hata hivyo, alisema matukio kama hayo ya samaki kukutwa ufukweni wakiwa wamekufa wakati mwingine hutokea wanapokosa hewa ya Oksijeni baharini.

Alisema mpaka sasa hawajapata taarifa za kuwapo kwa samaki wakiwa wamekufa sehemu nyingine zaidi ya ufukwe uliopo karibu na Hospitali ya Aga Khan.

Habari Kubwa