Same yaongeza kasi vitambulisho vya matibabu kwa wazee

13Jan 2018
Godfrey Mushi
 SAME  
Nipashe
Same yaongeza kasi vitambulisho vya matibabu kwa wazee

WILAYA ya Same, mkoani Kilimanjaro inakaribia kuipiku rekodi ya Halmashauri ya Ubungo ya Dar es Salaaam kwa kasi ya utoaji wa vitambulisho vya wazee kwa ajili ya matibabu bure, baada ya kusajili wazee 6,337.

Mkuu wa wilaya hiyo, Rosemary Staki.

Mkuu wa wilaya hiyo, Rosemary Staki, alisema awamu ya kwanza ya utekelezaji wa agizo la Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, umeifanya wilaya yake kuikaribia Ubungo ambayo hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana, ilikuwa imetoa vitambulisho hivyo kwa wazee 7,299.

“Huenda sisi tukawa wa pili kitaifa kwa kuendesha mchakato huu wa utoaji wa vitambulisho vya wazee, kwa sababu tofauti yetu na Ubungo ni wazee 962. Utaratibu huu kwa Wilaya ya Same utawasaidia wazee kuondokana na changamoto za kipato ambacho huwafanya washindwe kufikia huduma muhimu za tiba,” alisema.

Kwa hali ilivyokuwa kati ya mwaka 2015/2016, wengi wao hasa wale wanaoishi vijijini walikuwa bado wakitegemea msaada wa kufikia gharama za matibabu na mahitaji mengine muhimu ya kibinadamu kutoka kwa wasamaria.

Licha ya kuipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Same kwa hatua hiyo, Rosemary ametoa rai kwa madaktari na wauguzi, kuendelea kuwahudumia wazee wenye vitambulisho na wasiokuwa navyo, waangaliwe umri wao na wapewe huduma wanapofika hospitalini.

Wakati kundi kubwa la wazee wasiojiweza wakiendelea kuhitaji misaada, bado taifa lina deni kubwa la changamoto ya kukwama kwa miaka 15, Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 1999 ambayo haijapelekwa Bungeni mpaka sasa ili kutungwa na kuwa sheria.

Aidha,  alisema katika mwaka wa fedha 2017/2018, wilaya hiyo ilipokea fedha za dawa na vifaa tiba Sh. 510,505,630 na kwamba kiasi hicho ni sawa na ongezeko la asilimia 325.

Fedha hizo ni tofauti na ahadi ya Rais John Magufuli ambaye mwaka jana, aliipatia Wilaya ya Same vitanda 20 vya wagonjwa, vya kujifungulia vitano na magodoro 20 ili kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wa wilaya hiyo. 

 

Habari Kubwa