Samia aiagiza TAKUKURU kuandaa mfumo madhubuti kupambana na rushwa

28Mar 2021
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe Jumapili
Samia aiagiza TAKUKURU kuandaa mfumo madhubuti kupambana na rushwa

​​​​​​​RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan,  ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) kuandaa mfumo madhubuti wa kupambana na rushwa kwani vitendo hivyo bado vinaendelea katika maeneo mbalimbali.

​​​​​​​Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

 

Samia ameyasema hayo leo mara baada ya kupokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na taarifa ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) Ikulu Chamwino, Jijini Dodoma.

“Serikali itaendelea kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa kwani vitendo hivyo vimezidi kuendelea hivyo ni lazima kuwe na mikakati na mifumo mipya ya kukabiliana navyo” amesema Rais Samia.

Aidha Samia amesema atasimama imara katika mapambano dhidi ya rushwa hasa rushwa ya ngono ambayo imeonekana kukidhiri katika maeneo mengi.

Pamoja na hayo amemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Dr. Charles Kichere kutokuwa na kigugumizi chochote kwenye shirika analoona halifanyi vizuri kimapato.

“Tukinyamaziana kwa kutazamana sura hatutarekebisha na tutawaumiza Wananchi, naomba sana ripoti yako CAG iwe wazi zaidi, utakaponiletea ukaguzi wa mashirika naomba uwe wazi zaidi ili tujue tunachukua hatua gani” amesisitiza Samia.

Habari Kubwa