Samia afungukia wazee Dar

14Feb 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Samia afungukia wazee Dar

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amesema mambo yanayofanywa na serikali ya awamu ya tano ya Rais John Magufuli si nguvu ya soda kama ambavyo baadhi ya watu wanaweza kufikiri.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan

Aliyasema hayo jana wakati akizungumza kwenye mkutano ulioandaliwa na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya kuzungumza na Rais Magufuli, kuhusu mambo aliyoyafanya katika siku 100 za kwanza za utawala wake.

Samia alisema wale wanaodhani kuwa yanayofanyika sasa ni nguvu ya soda wakidhani ipo siku moto huo utapoa, watasubiri sana kwani kasi ya serikali itaendelea kuwa ile ile mwanzo-mwisho.

“Sisi siyo nguvu ya soda na wanaodhani hivyo basi watuangalie lakini nawathibitishia kwamba kasi ya serikali itaendelea kuwa ile ile,” alisema Makamu wa Rais.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema yeye na Baraza la Mawaziri wanawapenda watanzania na wataendelea kuwatumikia kwa nguvu na kwa moyo wao wote wakati wa awamu ya tano.

Alisema watawatumikia na kuwahudumia watanzania hivyo hawana haja ya kuwa na wasiwasi kuhusu utumishi wao, kwasababu watajitahidi kutimiza malengo ambayo wamewekewa na Rais Magufuli na Makamu wake, Samia Suluhu.

“Sisi tutakuwa watumishi wa watu; tunajua mnayoyataka na tutafanya hayo hayo ambayo watanzania mnayataka ili kuhakikisha tunakidhi mahitaji ya watanzania kwa kupata huduma bora za kijamii,” alisema Majaliwa.

Akizungumza awali kwenye mkutano huo pia, Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick alisema umejipanga kujenga madarasa 500 ili kuziba pengo lililosababishwa na mafuriko ya wanafunzi kwenye shule mbalimbali za msingi, kulikotokana na sera ya elimu ya bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne.

Sadick alisema ongezeko la wanafunzi limetia fora kiasi cha kusababisha kwenye baadhi ya shule wanafunzi kusomea nje ya madarasa kutokana na upungufu huo uliojitokeza.

Alisema baada ya kusikia kuwa elimu itakuwa bure, wazazi wengi waliamua kwenda kuwaandikisha wanafunzi hata ambao umri wao wa kwenda shule ulishapita hivyo kusababisha kwenye baadhi ya madarasa wanafunzi kufurika.

Alisema kwenye baadhi ya shule, wastani wa wanafunzi kwenye darasa moja ni kati ya 250-400 jambo ambalo mwisho wa siku litawasumbua walimu katika kuwapa elimu bora wanafunzi hao, na kuahidi kuwa Mkoa umejipanga kutatua kero hiyo.

“Hatulalamikii changamoto hii bali tumejipanga kuongeza idadi ya madarasa na shule mpya ili kuzifanya shule zilizojaa zipumue na kwa kuanzia tutajenga madarasa 500 na shule mbili mpya jirani na shule ambazo zimejaa idadi kubwa ya wanafunzi,” alisema.

Alisema baadhi ya shule kama Shule ya Msingi Majimatitu iliyoko Manispaa ya Temeke ilitarajia kuandikisha wanafunzi 400 lakini kutokana na hamasa ya wazazi baada ya kusikia kuwa elimu itatolewa bure, wameandikisha 1022 mwaka huu.

Habari Kubwa