Samia ahimiza wanawake zaidi wajumuishwe ujumbe wa bodi

25Feb 2016
Mary Geofrey
Dar
Nipashe
Samia ahimiza wanawake zaidi wajumuishwe ujumbe wa bodi

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ameyataka mashirika mbalimbali nchini kuwaingiza wanawake kwenye nafasi za ujumbe wa bodi.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan,akifungua mpango wa kutoa mafunzo ya uongozi kwa wanawake.

Aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akifungua mpango wa kutoa mafunzo ya uongozi kwa wanawake, namna ya kufanya kazi, kuongoza nafasi za ukurugenzi na bodi mbalimbali ujulikanao kama ‘Female Future Tanzania’ ulioandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE).

Alisema katika taasisi na mashirika binafsi,
idadi ya wanawake wanaoingia kwenye nafasi za juu kama wakurugenzi na wajumbe wa bodi, imekuwa ikiongezeka.

“Serikali kupitia Katiba inayopendekezwa inaeleza nafasi za wanawake na wanaume kuwa ni 50 kwa 50...nafikiri muda mwafaka kwa wanawake kupata elimu hii ya namna ya kuongoza ili kujengeana uzoefu na kuendelea kukuza uchumi wa taifa kupitia taasisi wanazozitumikia,” alisema.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ATE, Zuhura Muro, alisema mpango huo walioufungua rasmi kwa kushirikiana na Shirika la Waajiri nchini Norway (NHO), utawezesha wanawake kupata mafunzo ya namna ya kusaidia kuwa wakurugenzi wa bodi na kuingia kwenye nafasi za kufanya uamuzi mkubwa.

Alisema mafunzo hayo yataanza kutolewa kwa walimu kuhusu uongozi na namna ya kufanya kazi kwenye bodi za kurugenzi mbalimbali kabla ya wao kwenda kuwafundisha wanaotaka kupata mafunzo hayo.

“Mpango huu tunaamini utakuwa na manufaa makubwa sana kwa sababu katika bodi nyingi za mashirika, wanawake ni wachache hivyo kuongeza idadi yao ndani yake kutasaidia kuongeza ufanisi katika biashara na taasisi,” alisema.

Aliongeza kuwa mpango huo utaanza mara taratibu za washiriki kujiorodhesha na walimu kupewa mafunzo kutoka kwa wataalam waliojifunza kutokea Norway.

Alisema kwa upande wa Afrika, Tanzania ni ya tatu kuanzisha mpango huo baada ya kutanguliwa na Uganda mwaka 2012 na Kenya mwaka 2013.

Habari Kubwa