Samia akemea Tanzania kuwa dampo bidhaa feki

03Jul 2019
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Samia akemea Tanzania kuwa dampo bidhaa feki

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ameonya Tanzania kuwa dampo la bidhaa hafifu huku akisisitiza kuwa serikali haitakubali kuruhusu bidhaa za nje zisizo na ubora kuingia nchini.

Samia alisema hayo jana wakati akifungua Maonyesho ya 43 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF) yanayoendelea katika Viwanja vya Maonyesho ya Mwalimu Nyerere, Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam.

Ili kuhakikisha mianya inazibwa, aliiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara kudhibiti kuingia kwa bidhaa zisizo na ubora kutoka nje ili kuzipa nafasi bidhaa za ndani.

Alisema ni vyema ikahakikisha bidhaa zinazotoka nje zinakuwa zenye ubora tu ambazo zina uwezo wa kuleta changamoto kwa bidhaa za ndani.

"Viwanda vya ndani vina uwezo wa kuzalisha bidhaa bora zinazokidhi mahitaji ya soko la ndani, lakini changamoto ni kuwapo kasumba ya Watanzania kupenda kutumia bidhaa za nje kuliko za ndani ilhali bidhaa zetu zina ubora unaojitosheleza," alisema.

"Tunachotaka ni kuhakikisha Wizara ya Viwanda (na Biashara) inasimamia wazalishaji kuongeza thamani na kuboresha zaidi bidhaa zetu kuwa za kisasa ili ziuzwe na nje."

Alisema baada ya bidhaa kuongezewa thamani, balozi za Tanzania nje ya nchi zitapata kazi ya kutafuta masoko.

Samia pia aliziagiza mamlaka zinazohusika na upatikanaji wa malighafi kuhakikisha zinazalisha zile zitakazokidhi mahitaji ya viwanda vya ndani.

Alisema kwa kufanya hivyo viwanda vya ndani vitakuwa na uhakika wa soko la ndani na nje, na kusaidia kuongeza akiba fedha za kigeni.

Pia aliziagiza mamlaka zinazohusika kusimamia utekelezaji wa mpango wa kuboresha mfumo wa udhibiti wa biashara nchini (Blueprint) ikiwamo Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu (GCLA), Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Maliasili na Utalii, kusimamia utekelezaji wake.

"Tunataka mamlaka husika zisimamie kwa nguvu zote utekelezaji wa ‘Blueprint’ na tutazisimamia kwelikweli kuhakikisha zinaleta mrejesho mara kwa mara wa udhibiti wa vikwazo vya biashara ili pale penye tatizo tuwe tunalishughulikia," alisema.

Makamu wa Rais alisema maonyesho hayo yamethibitishwa kuwa bora katika Kanda ya Afrika Mashariki na Kati, hivyo kampuni zitumie fursa hiyo kujitangaza zenyewe, fursa za utalii na uwekezaji.

Naye Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, alisema wako katika mkakati wa mapitio ya sera ambayo yataendana na uchumi wa viwanda na kukamilika ifikapo mwakani.

Alisema mwitikio wa maonyesho hayo kwa mwaka huu umeongezeka na idadi ya kampuni za nje zinazoshiriki kufikia 580 kutoka 508 mwaka jana.

Habari Kubwa