Samia apata dawa kukomesha ukatili

24Oct 2021
Julieth Mkireri
RUFIJI
Nipashe Jumapili
Samia apata dawa kukomesha ukatili

RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka wanawake kuungana kupinga ukatili unaofanywa dhidi yao.

Alitoa rai hiyo jana alipohutubia kwenye maadhimisho ya kilele cha Wiki ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) yaliyofanyika Ikwiriri wilayani Rufiji mkoani Pwani jana.

Alisema lipo ongezeko la vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake ambapo wanawake wamekuwa hawapazi sauti ipasavyo kukomesha vitendo hivyo.

"Ninadhani wanawake tunachangia kwa sababu linapotokea tunalikingia kifua, haipendezi kukuta mwanamke mwenzio anadhalilishwa nawe ukasimama kulitetea kwa sababu aliyefanya kitendo hicho ni ndugu au kaka yako," alionya.

Rais aliwataka wanawake kubadilika na kusema yale yaliyo mazuri na kuacha na kusemeana mambo ya uongo, wapendane na kushirikiana katika kumkomboa mwanamke kiuchumi na kifikra.

Rais Samia pia alitoa rai kwa watafiti na waandishi wa sayansi ya historia kuandika kuhusu Bibi Titi Mohamed.

"Wangapi wana ujasiri wa kuwaunganisha wanawake wa Kitanzania kupata ukombozi wa kifikra? Tunatakiwa kuyaenzi yale yaliyofanywa na Mwenyekiti wa kwanza wa UWT, Bibi Titi Mohamed," alisema.

Mwenyekiti wa UWT Taifa, Gaudensia Kabaka, aliwataka wanawake kumpa ushirikiano Rais Samia katika utekelezaji wa majukumu yake ili kupata matokeo ya haraka.

Katibu Mkuu wa UWT, Phills Nyimbi, alisema jumuiya hiyo inampongeza Rais kwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati na utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge, alimshukuru Rais Samia kwa kutenga fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika mkoa huo.

Kunenga alisema serikali imetoa Sh. bilion 21 kwa ajili ya miradi ya maji inayotekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).

Pia alishukuru ongezeko la bajeti ya barabara za mjini na vijijini kutoka Sh. bilioni tisa mwaka 2020/21 hadi Sh. bilioni 43 mwaka huu.

Mbunge wa Rufiji, Mohamed Mchengerwa, aliipongeza jumuiya hiyo kufanya maadhimisho hayo katika jimbo hilo na kujenga mnara wa kumuenzi Bibi Titi Mohamed.

Habari Kubwa