Samia ataja mafanikio ziara za nje

19Oct 2021
Cynthia Mwilolezi
Arusha
Nipashe
Samia ataja mafanikio ziara za nje

RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa ziara zake nje ya nchi ni kwa ajili ya Watanzania na sio kwa lengo la kutembea kwenye nchi hizo.

Akihutubia wananchi jijini Arusha juzi, alisema ziara chache alizofanya nchi mbalimbali zimesaidia kuondoa vikwazo na kuogeza wigo kwa wafanyabiashara nchini.

“Ziara nilizokuwa nikifanya nchi jirani madhumuni ilikuwa kuondoa vikwazo, kunyoosha njia ili wafanyabiashara wetu waweze kuuza ndani na nje, tumeondosha vikwazo na nchi ya Kenya, naambiwa biashara imekuwa mara sita kuliko wakati wa vikwazo,” alisema na kuongeza;

“Tukizunguka (ziara za nje) hivi msiseme mama (Rais) anazunguka tu, sitazunguka bila sababu, nilishacheza vya kutosha kwenye nchi nyingi duniani, sasa hivi kazi ni moja tu kuzunguka kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania.”

 

KUPANDA SARUJI, MABATI

Rais Samia alithibitisha kupanda kwa bei ya saruji na mabati na tatizo baadhi ya wazalishaji waagiza malighafi nje ambako kulikuwa kumefungwa kutokana na Uviko-19.

“Nimemwagiza Waziri wa Viwanda na Uwekezaji awaite wazalishaji wa saruji, nondo, mabati na vifaa vingine vya ujenzi kwa sababu fedha (Uviko-19) tulizipitisha juzi za ujenzi wa madarasa zaidi ya 15,000 kama vifaa hivyo vitakuwa bei juu mradi wetu utafeli, tunawataka wazalishe bidhaa kwa wingi ili wananchi wapate na bei ishuke,” alisema.

AKUSANYA MABANGO

Akiwa Usa River kuelekea jijini Arusha, Rais Samia aliagiza mabango yote waliyokuwa wamebeba wananchi yakusanywe na akaahidi kwenda kuyasoma yote.

 

MAJI, BARABARA

Alisema changamoto kubwa ya Mkoa wa Arusha ni barabara na maji na kwamba kitakachofanyika ni kukaa mkoa na wilaya zake ili kuangalia barabara za kipaumbele kuanza nazo kwa zilizoko chini ya TANROADS na TARURA.

“Tunataka zipitike muda wote mazao yatoke shambani kwenda kwenye masoko, tutajipanga vizuri kuangalia wapi kuanze na wapi tumalizie, tunaunganisha wilaya kwa wilaya, kuondoa barabara za vumbi. Miradi ya maji tumeishughulikia inaendelea kukamilika,” alisema.

Akiwa jijini Arusha, alisema serikali itafufua viwanda ili kutoa ajira kwa wingi na kukuza uchumi, huku akisema wanarudisha hadhi ya Tanzanite ijulikane inatoka Tanzania na sio kuacha itoke holela bila nchi kuona faida.

Rais Samia alisema kwa muda mrefu watu wengi duniani wanajua madini hayo yanapatikana nchi nyingine badala ya Tanzania na kuahidi kwamba kwa sasa wanairudishia hadhi na kuna udhibiti ili nchi ione manufaa.

“Tukiachia itoke inavyotoka itakwisha bila kuona thamani yake, kwa sasa tunadhibiti tunaitoa kwa viwango, tunaangalia mahitaji ya ulimwengu na bei ya Tanzanite itapanda kwa sababu tunatengeneza chache katika kupeleka duniani na thamani yake itapanda na nchi itanufaika, na sasa tuna hesabu imechangia kiasi gani kwenye uchumi wetu,” alisema.

 

MIKOPO YA NJE

“Nawaahidhi Watanzania nitaangalia mikopo yenye unafuu kwa nchi yetu, inayoleta faida kwa nchi yetu, mikopo chechefu sitaichukua ila inayoleta nafuu na maendeleo sitaiogopa nitaichukua,” alisema.

VIWANDA

Alisema serikali imejipanga kuanzisha kongamano la viwanda na kwa sasa wanamalizana na mwekezaji wa kiwanda cha matairi ya General Tyre, kwa kuwekeza viwanda zaidi ya 20 ikiwamo cha kutengeneza mpira.

“Viwanda ni ajira kwa Watanzania, serikali iko kwenye mpango wa kuviandalia viwanda vilivyofungwa ni ukweli hata vikifufuliwa leo haviwezi kufanya kazi iliyofanyika wakati huo ndiyo maana tumekuja na kongano za viwanda kila eneo lililofaa ili kukuza ajira na uchumi wa taifa,” alisema.

Alihidi kushughulikia migogoro ya ardhi, ujenzi wa barabara kwa ajili ya kuharakisha maendeleo na mkopo wa kushughulikia utalii, afya na elimu.

“Tunataka kuhakikisha matatizo yote yanayowakabili wananchi tunayashughulikia ipasavyo, tuna tatizo la wafanyabiashara wadogo na masoko, yote tunayafanyia kazi ili wananchi waondokane na kero…lengo letu ni kuwahudumia wananchi, tunachowaomba amani na utulivu serikali yenu ipo na kwa ajili ya wananchi,” alisema.

Habari Kubwa