Samia ataka wazalendo uwekezaji viwanda ndani

07Dec 2021
Jenifer Gilla
Dar es Salaam
Nipashe
Samia ataka wazalendo uwekezaji viwanda ndani

RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka wawekezaji wa ndani kuchangamkia fursa ya uwekezaji katika viwanda, ikiwa ni njia mojawapo ya kujikwamua kiuchumi kwa kuepuka utegemezi wa kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi.

Rais Samia Suluhu Hassan akikata utepe kuzindua rasmi awamu ya kwanza ya kiwanda cha vifaa vya umeme cha Elsewedy Electric East Africa Ltd kilichoko Kisarawe II Kigamboni jijini Dar es Salaam jana. PICHA: IKULU

Aliyasema hayo jana wakati akizindua kiwanda cha nyaya za transfoma na umeme cha El Sewedy kilichoko Kisarawe, Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam kilichojengwa na wawekezaji kutoka Misri.

“Tunaposherehekea siku hii muhimu na adhimu (miaka 60 ya Uhuru) ni lazima kutafakari maazimio yetu tuliojiwekea mwaka 1961 ya kujikomboa kiuchumi, kwa kuondoa utegemezi wa kuagiza bidhaa kutoka nje na kuongeza uzalishaji wa ndani,” alisema.

Rais alisema kiwanda hicho kitazalisha bidhaa za teknolojia ya hali ya juu kwa kuzalisha tani 15,000 za nyaya za umeme, transfoma 1,500 na mita za 100,000 za umeme kwa mwaka.

“Nusu ya bidhaa hizi zitauzwa masoko ya nje na kuongeza ujazo wa pesa za kigeni, aidha kinachobaki kitatumika nchini na kuondoa utegemezi wa bidhaa za nje,” aliongeza.

VIWANDA KIGAMBONI

Alisema pia Wilaya ya Kigamboni itakuwa eneo maalum la uwekezaji ambapo wawekezaji wataelekezwa kujenga viwanda vyao huko.

“Kwa hiyo Kigamboni sasa linakuwa eneo maalum ambapo wawekezaji wataelekezwa kuja kama mlivyosikia, tutakuwa na industrial city (mji wa viwanda) ambao utakuwa na uwekezaji mwingi ndani yake.”

Aliahidi kushughulikia changamoto za maji, umeme na barabara zinazoikabili wilaya hiyo ili kunyoosha njia ya uwekezaji.

“Natambua katika eneo hili kuna changamoto ya barabara...na kwa sababu tunafungua Kigamboni kuwa eneo la viwanda pia, kipaumbele cha kwanza kitatolewa kuhakikisha maeneo yote yana umeme, yana maji na barabara za lami, ” alisema.

“Ndugu zangu niwasihi sasa wote wanaonisaidia, tuachane na mtindo wa kazi tuliozoea, kama tulikuwa tumezoea uwekezaji wa Dola milioni nane, milioni tisa, sasa wanaokuja ni wa madola mengi mengi,” alisema Rais Samia.

Alisema pia ziangaliwe fursa chanya zinazopatikana katika janga la Covid-19 kufunguka kiuchumi.

“Maradhi haya ya Covid-19 upande mwingine ni mabaya upande mwingine yametoa fursa kwa Bara la Afrika kufunguka kiuchumi, mapinduzi ya nne ya viwanda yamefungua Bara la Afrika, lakini maradhi haya yamefungua zaidi ...kwa kudra za Mwenyezi Mungu Dar es Salaam tumewekwa pazuri...kama lango la kuingilia Afrika yote,” alifafanua.

Aliwashukuru wageni 111 kutoka Misri wakiwamo wawekezaji wakubwa 40 waliokuja kuangalia fursa za uwekezaji nchini na kumsisitiza Waziri wa Uwekezaji, Godfrey Mwambe, kuwaonyesha fursa.

Mkurugenzi wa Kiwanda hicho Afrika Mashariki, Ibrahim Kamal, alisema nyaya za umeme na transfoma zinazotengezwa kwa kiwango cha juu, kati na chini, kitanufaisha wakazi wa vijini na vijijini na kinatarajia kutoa fursa ya ujuzi wa masuala ya umeme kwa Watanzania na ajira 500.

Habari Kubwa