Samia atangaza neema Tabora,fursa ujenzi kiwanda cha asali

20May 2022
Halfani Chusi
Nipashe
Samia atangaza neema Tabora,fursa ujenzi kiwanda cha asali

RAIS Samia Suluhu Hassan, amewataka wananchi mkoani Tabora, kuchangamkia fursa za ajira kupitia miradi inayoendelea mkoani humo.

RAIS Samia Suluhu Hassan.

Pia amewaahidi Mkoa wa Tabora utakuwa alama ya asali ndani na nje ya nchi kupitia kiwanda kikubwa kinachotarajiwa kujengwa mkoani humo.

Aliyasema hayo jana wakati akihitimisha ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani humo ambayo ilienda sambamba na ufunguzi wa barabara.

Akiwa mkoani humo, Rais Samia aliwataka wananchi wa mkoa wa Tabora kuwa walinzi wa miundombinu inayojengwa ikiwamo barabara, reli na kiwanda cha kusindika asali kinachotarajiwa kuanza kujengwa hivi karibuni.

Rais Samia alisema Tabora imekuwa miongoni mwa mikoa yenye rasilimali nyingi, hivyo serikali haina budi kupeleka maendeleo mkoani humo.

“Ukiangalia mkoa wa Tabora kuna ardhi ya kutosha kwa kilimo, lakini kuna hifadhi za misitu ambayo imekuwa ikisaidia upatikananji wa asali. Kwa hiyo niseme tu fedha ambazo zimetolewa kwa ajili ya miradi inayoendelea huku zikatumike ipasavyo kwa kuzingatia kanuni na sheria za nchi,” alisema.

Katika hatua nyingine, Rais Samia aliwaagiza wakuu wa halmashauri zote nchini kuwa wakweli na wawazi kwa wananchi pindi wanapopewa pesa kwa ajili ya kusimamia miradi.

“Fedha za halmashauri zitumike kwa uwazi lakini inapaswa wananchi wajue ni kiasi gani kimetolewa kwa ajili ya mradi husika na wakijua wataweza kufatilia kwa kuangalia mradi na pesa iliyotumika je inafanania,” alisema na kuongeza:

“Kwenye fedha za seriali lazima kanuni za fedha zifuatwe. Pesa za serikali zinahitaji nidhamu siyo za mtu binafsi.

Pamoja na mambo mengine, Rais Samia aliwaahidi wananchi wa Mkoa wa Tabora kumaliza kero mbalimbli zinazowakabili kama inavyosema ilani ya uchaguzi.

Habari Kubwa