Samia atoa salamu za pole kufuatia kifo cha waziri wa ulinzi

03Aug 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Samia atoa salamu za pole kufuatia kifo cha waziri wa ulinzi

Rais wa Samia Suluhu Hassan, ametuma salam za pole kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Venance Mabeyo, kufuatia kifo cha Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Elias Kwandikwa.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Jaffar Haniu imeeleza kuwa Rais amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo hicho kutokana na mchango wake mkubwa katika utumishi wa umma.

Kwandikwa ambaye pia ni Mbunge wa Ushetu Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, alifariki dunia usiku wa Jumatatu Agosti 2, 2021 akiwa hospitalini jijini Dar es Salaam.

“Tumempoteza mtu muhimu ambaye mchango wake katika utumishi wa umma hautasahaulika, Kwandikwa alikuwa kiongozi shupavu ambaye alikuwa akitekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria na taratibu,” amesema Samia.

Samia amemtaka Jenerali Mabeyo kufikisha salam zake za pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na watu wote walioguswa na msiba huo.