Samia awaasa vijana kujiunga mabaraza ya vijana

12Jan 2018
Rahma Suleiman
Nipashe
Samia awaasa vijana kujiunga mabaraza ya vijana

MAKAMU wa Rais,  Samia Suluhu Hassan, amewataka vijana kuwa na utamaduni wa kujiunga na mabaraza ya vijana ili waweze kunufaika na fursa za mikopo ya kujikwamua na umaskini.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, akihamasisha vijana wakati wa Uzinduzi wa Baraza la Vijana Zanzibar, akiwa pamoja na Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto, Maudline Cyrus Castico (kulia kwake), uliofanyika kwenye mjini Zanzibar juzi. PICHA: OMR

Akizungumza katika uzinduzi wa Baraza la Vijana Zanzibar, Samia alisema  kuna faida nyingi zinazopatikana katika mabaraza ya vijana hivyo ni vyema kwa vijana kujiunga.

Alisema vijana ndio hazina ya taifa kwa sababu ndio kundi kubwa lenye nguvu na linaweza kukuza uchumi na kuleta maendeleo ya nchi.

Alisema kundi hilo ni jepesi kubadilika na linaweza kutumika kwa wema au kwa uovu na pia ni hazina kwa sababu ni jepesi kujifunza kulingana na mazingira yaliyopo. Alisema kwa kuzingatia hayo ndio maana mataifa yote duniani yanakuwa na utaratibu maalum kwa ajili ya kundi la vijana ili kulijengea mazingira bora na mustakabali wao na kwa taifa kwa ujumla.

Alisema kuwa kuna kundi kubwa la vijana halijajiunga na mabaraza ya vijana hivyo aliwataka kuwashawishi vijana wenzao kujiunga katika mabaraza ili kuendelea kujadii na kuongeza kasi ya kutetea maslahi yao na lengo la kuanzishwa mabaraza ya vijana ni kuwajengea uwezo wa kujitambua na kuwa watetezi wa nchi. 

Habari Kubwa