Samia awaonya wanaotolea macho fedha za halmashauri

18May 2022
Halima Ikunji
TABORA
Nipashe
Samia awaonya wanaotolea macho fedha za halmashauri

RAIS Samia Suluhu Hassan amewaonya wakurugenzi wa halmashauri nchini wasizitolee macho fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya wananchi na kwamba watakaothubutu 'kuzidokoa' watakiona cha moto.

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait (KFED), Waleed SH. Albahar, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi Dk. Batilda Buriani na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini TANROADS, Mhandisi Rogatus Mativila, akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Barabara ya Nyahua-Chaya yenye urefu wa kilomita 85.4, Tura, Uyui, mkoani Tabora jana. PICHA: IKULU

Alitoa kauli hiyo jana katika sherehe za ufunguzi wa barabara ya Nyahua-Chaya yenye urefu wa kilometa 85.4 akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani hapo.

Rais Samia alisema fedha zote za miradi zinatakiwa kutumika ipasavyo na kama ilivyoelekezwa na serikali ili wakurugenzi hao waepukane na mkono wa mrefu wa serikali.

Alisema serikali inatambua kilio cha wananchi na ndiyo maana inajitahidi kila hali kuhakikisha inatekeleza na kutataua shida zao.

Aidha, alisema serikali itaendeleza miradi yote iliyoanzishwa pamoja na kutafuta fedha zingine kwa ajili ya kuhakikisha kila kitu kinakamilika.

Alisema amesikia kilio cha wananchi wa Wilaya ya Uyui na ametoa fedha kwa kushirikiana na Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait Sh. bilioni 123 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo.

Katika hatua nyingine

Rais Samia aliwataka wananchi wasing’oe alama za barabarani ambazo zitawasaidia madereva kuona mbele kuna kitu gani ili kuepusha ajali zinazoendelea kutokea sehemu mbalimbali nchini.

Kadhalika walitakiwa kutunza miundombinu ya barabara na kuonya kufanya hivyo kutasababisha ajali kila siku katika barabara hiyo.

Alisisitiza lengo la serikali ni kuhakikisha barabara zote zinajengwa kwa kiwango cha lami katika maeneo yote yaliyobakia na kuiagiza Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kuhakikisha wanafanya kazi hiyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk. Batilda Buriani, akitoa taarifa fupi mbele ya Rais alisema, Wilaya ya Uyui inazalisha asali ambayo inawapatia kipato wakazi wa eneo hilo.

Alisema katika fedha zilizotolewa za Uviko-19 zimetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Mkoa wa Tabora na wilaya zake.

Balozi huyo alimshukuru Rais kwa ujio wake na kutoa fedha kwa ajaili ya ujenzi huo wa barabara yenye urefu wa kilometa 85.4 kutoka Nyahua hadi Chaya.

Alisema katika fedha za UVIKO - 19 zilizotolewa zilitumika katika ujenzi wa vyuo vya ufundi katika Wilaya ya Uyui na Igunga mkoani humo.

Dk. Buriani aliahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kushirikiana na viongozi wenzake ili kuleta maendeleo kwa jamii.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Igalula mkoani Tabora, Venanti Daudi, alimwomba Rais Samia kusaidia ujenzi wa barabara ya kutoka Mpakani mwa Tabora hadi Tura.

Alisema kwamba katika jimbo lake, vijiji 48 havina umeme jambo ambalo linarudisha nyuma shughuli za maendeleo kwa wananchi wake.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, alimweleza Rais Samia kuwa Mfuko wa Barabara utaendelea kuboreshwa kila mwaka ili kuboresha miundombinu ya barabara katika mikoa yote nchini.

Habari Kubwa