Samia: Kuna kundi linaichafua serikali

05Dec 2021
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Samia: Kuna kundi linaichafua serikali

​​​​​​​RAIS Samia Suluhu Hassan amesema kuna makundi yanaichafua serikali ya awamu ya sita ionekane ufisadi umerudi na mambo yako ovyo, akisisitiza hatakubali na atasimamia haki za wananchi.

​​​​​​​RAIS Samia Suluhu Hassan

Mkuu wa Nchi alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akizindua gati katika Bandari ya Dar es Salaam, akionya: "Kuna makundi wanajua wanayoyafanya ndani ya serikali. Ni makundi hayo hayo yanageuka kusema serikali ya awamu ya sita ufisadi umerudi, mambo yako ovyo, kumbe wao ndio wako ovyo."Na mambo yale hayakufanyika ndani ya awamu ya sita, yalifanyika huko nyuma, gari bovu linaangushiwa awamu ya sita. Sitakubali, sitakubali! Niliapa kusimamia haki za wananchi, nitasimama nao, nitasimama kutetea haki za wananchi, sitakubali!"Katika utekelezaji wa ahadi yake hiyo kwa wananchi, Rais Samia alitangaza kuzivunja Bodi ya Mamlaka ya Badari Tanzania (TPA) na ile ya Shirika la Meli kwa kuwaondoa wenyeviti wake kutokana na kutoridhishwa na utendaji wao wa kazi.Rais Samia pia aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuchunguza dosari zilizojitokeza katika taarifa ya uchunguzi ya mifumo ya kielektroniki katika bandari ya Dar es Salaam na kuchukua hatua stahiki."TAKUKURU ninaagiza, ninatoa amri uchukue hatua dhidi ya watu hawa haraka na kama ripoti hii hamna, nitawapatia ya nini kilichofanyika hapa, watu waliofanya hayo wapo bado ofisini. Watu tunachekeana tu, tunatizamana tu."Watu wapo maofisini wanaendeleza wizi na ubadhirifu wa mali za umma, mifumo imekuwa ikichezewa, inaonyesha kuwa mizigo imelipiwa kutoka getini, lakini siyo kweli, haijalipiwa hivyo bandari kukosa mapato. Haya mapato yanayoonekana leo hayakupaswa kuwa hivyo yalivyo," alisema.Alisema kumekuwa na dosari ya kuwapo mianya mingi ya upotevu wa mapato inayotokana na kukataa kwa makusudi kuweka mifumo madhubuti ya ukusanyaji mapato na mifumo inayosomana baina ya bandari na Mamlaka ya Mapato (TRA).“Mapato katika Bandari ya Dar es Salaam yamekuwa yakipanda na kushuka na kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2019/20, bandari ilikusanya Sh. bilioni 901, mwaka 2020/21 ilikusanya Sh. bilioni 896 na matarajio ya 2021/22 ni kukusanya Sh. bilioni 980,” alisema.Rais alisema licha ya baadhi ya 'madudu' hayo kuonyeshwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), mpaka sasa hakuna hatua zilizochukuliwa na bado kuna mianya ya uvujaji wa mapato kutokana na mifumo ya malipo kuchezewa na wafanyakazi.Alimkumbusha Mkurugenzi wa Bandari kuwa alimpeleka huko kusimamia na kudhibiti mapato ya mamlaka hiyo, akibainisha kuwa mambo yote yanatokea wakati Bodi ya Wakurugenzi wa Bandari ipo.“Ipo kampuni iliingia mkataba wa Sh. milioni 694 na ililipwa Sh. milioni 600 lakini haikumaliza kazi iliyotakiwa na mkataba ukavunjwa, fedha zilikwenda bila kazi kufanywa, ripoti pia ilieleza kuwa utaratibu wa kutoa zabuni hizo haukufuatwa,” alisema.WAZIRI KIKAANGONIRais Samia alimtaka Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa kufanya marekebisho na kama hawezi amfuate wakae kikao cha pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi kuona namna ya kufanya marekebisho kwenye wizara.“Kasimamie kazi hii kama ninavyotarajia na utakaposhindwa njoo niambie 'dada nimeshindwa', nitaangalia mwingine ambaye labda ataweza kunisaidia lakini haya hayawezi kuendelea,” Rais Samia alionya.WAHUJUMU MIUNDOMBINUKatika hatua nyingine, Rais Samia alisema jana kuwa licha ya serikali kutoa fedha nyingi kutekeleza miradi, wananchi wachache wasio na uzalendo wanaihujumu kwa kuiba vifaa na mafuta ya mitambo ya ujenzi.Rais alitoa kauli hiyo wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka Mbagala wilayani Temeke, ambao ukikamilika utakuwa na watumiaji 673,800 kwa siku.“Kuhujumu miradi hii siyo jambo jema, ninawaomba sana wananchi mtakapogundua kuna watu wana hujumu miradi hii, muwaseme, msiwaonee aibu, nikemee vitendo hivi visivyo na afya wala maslahi kwa taifa, raia wote tuwe walinzi wa miradi hii,” aliagiza.Rais Samia aliagiza zifanyike doria za mara kwa mara katika maeneo hayo ikiwa ni pamoja na hatua za kisheria zichukuliwe kwa wote watakaobainika kufanya vitendo vya kuhujumu miundombinu.Pia aliitaka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Wakala wa Barabara (TANROADS) kuhakikisha kazi za ujenzi na ukarabati wa barabara na madaraja zinatekelezwa kwa viwango vilivyokusudiwa kimkataba ili zidumu kwa muda unaotarajiwa.Rais Samia alisema siku hizi hata kama mradi umechelewa kisingizio ni UVIKO-19, akisisitiza kuwa licha ya mlipuko wa baa hilo kwenye mradi huo kulikuwa na uzembe wa makandarasi na watendaji wa serikali, akiagiza umalizike kwa muda uliopangwa.“Mwezi Juni nilifanya ziara ndani ya wilaya ya Temeke, nikapita barabara ya mwendokasi, nikakuta ubovu ambao waziri umeutaja na nikaelekeza hatua zichukuliwe. Kwa ubovu ule kama viongozi wasingesimama na kusema hapa ni pabovu, mkandarasi angeendelea kutujengea kwa ubovu uleule," alionya.

Habari Kubwa