Samia: Mchakato Moshi kuwa jiji bado kidogo

16Oct 2021
WAANDISHI WETU
MOSHI
Nipashe
Samia: Mchakato Moshi kuwa jiji bado kidogo

RAIS Samia Suluhu Hassan, amewafungulia wakazi wa Mji wa Moshi kinachoendelea kuhusu Halmashauri ya Manispaa hiyo kupandishwa hadhi kuwa jiji, kwamba kuna mambo bado hayajakamilika.

Rais Samia Suluhu Hassan, akiondoa kitambaa kuzindua rasmi barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 32.2, katika eneo la Sanya Juu, wilayani Siha, mkoani Kilimanjaro jana. PICHA: IKULU

Akizungumza jana na wakazi hao kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Rais Samia, alitolea ufafanuzi suala hilo kutokana na ombi la kuharakisha mchakato huo lililoibuliwa awali mkutanoni. 

“Mji wa Moshi unadaiwa ili uwe Jiji, na Mji wa Vunjo nao wanataka kuwa Halmashauri, na kutoka Vunjo hadi Moshi ni takribani kilometa 20, Je, tuivunje Vunjo, iwe ndani ya litakalokuwa Jiji la Moshi?” Rais Samia alitamka katika ufafanuzi wake.

Aliahidi serikali kufanyia kazi suala hilo, katika hali inayoendana na ombi hilo lililoibuliwa mkutanoni na mmoja wa viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Juzi, akiwa katika mkutano wa hadhara mjini Chato, Rais Samia alitoa ufafanuzi unaofanana na wa jana kuhusu mji huo wa Kanda ya Ziwa, katika mchakato wake wa kuwa mkoa.

Akiwa wilayani Siha jana, Rais Samia alizindua barabara ya Sanya Juu/Elerai iliyojengwa kwa kiwango cha lami na Kampuni ya Kimataifa ya Geo Engineering ya China (CGC), ikigharimu zaidi ya Sh. bilioni 62.7.

Kwenye taarifa ya utekelezaji ujenzi wa barabara hiyo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Rogatus Mativila, alisema ujenzi wa barabara hiyo ulikamilika mwaka 2019 na inatarajiwa kudumu kwa wastani wa miaka 20.

Rais Samia Suluhu Hassan alisema tatizo kubwa lililoko Mkoa wa Kilimanjaro ni migogoro ya ardhi, huku akiahidi kuitatua haraka.

Alisema matatizo yote ambayo ameyaona kwenye mabango yenye jumbe mbalimbali ikiwamo migogoro ya ardhi, maji na maslahi ya wafanyakazi, ameyachukua na anakwenda kuyachambua na kuyafanyia kazi.

“Tunapita kuangalia yaliyotendeka na kuona matatizo yaliyopo na hapa ninaona mabango mengi. Kuna migogoro ya ardhi na maslahi ya wafanyakazi, ninaomba tuyakusanye yote halafu tutaenda kuyafanyia kazi.

"Changamoto hizi tutaenda kuzifanyia kazi na ahadi yetu Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kuangalia kero za wananchi na kuzifanyia kazi.

"Ninajua hapa Kilimanjaro kuna changamoto ya maji na migogoro ya ardhi ambayo ndio changamoto kubwa. Changamoto zote ambazo nimeziona kwenye mabango nitazichukua na kwenda kuzichambua na kuzifanyia kazi," alisema.

Vilevile, Rais Samia alisema baadhi ya wananchi wapo kwenye maeneo ya serikali na wanatakiwa kuondoka, akiahidi kuangalia namna bora ya kushughulikia dosari hiyo.

Rai yake kwa wakazi wa Kilimanjaro, waendelee kudumisha amani na utulivu ili serikali ipate wasaa wa kuangalia namna nzuri ya kushugulikia vikwazo vilivyopo.

*Imeandikwa na Godfrey Mushi na Anjela Mhando*

Habari Kubwa