Samia: Naona fahari, napata ari, ujasiri kuniunga mkono

21Nov 2021
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe Jumapili
Samia: Naona fahari, napata ari, ujasiri kuniunga mkono

​​​​​​​RAIS Samia Suluhu Hassan amesema anaona fahari jinsi Watanzania wanavyomuunga mkono katika uongozi wake, hatua ambayo inampa ari na ujasiri mkubwa wa kisiasa.

Rais Samia Suluhu Hassan, akipokea zawadi ya ngalawa kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Zanzibar, Swahiba Kisasi wakati wa mkutano ulioandaliwa na jumuiya hiyo, kwa ajili ya kumpongeza katika Viwanja vya Maisara Zanzibar jana. PICHA: IKULU

Alitoa kauli hiyo jana mjini Zanzibar alipohutubia mkutano wa hadhara uliotayarishwa na Umoja wa Wanawake (UWT) kwa ajili ya kumpongeza kufuatia mafanikio ya majukumu yake.

Alisema asili yake ni tunda linalotokana na malezi mazuri kutoka kwa viongozi wake ambao amepitia kwa nyakati tofauti, akimtaja Rais mstaafu Amani Abeid Karume kuwa ndiye aliyemfungulia mwanga wa kisiasa.

"Malezi niliyoyapata ni mazuri kwa walezi wangu na ndiyo maana ni sehemu ya mafanikio yangu ya safari za kisiasa ambapo Rais mstaafu Karume alifunguwa maisha yangu ya kisiasa," alisifu.

Alisema ataendelea kuongoza nchi kwa kufuata misingi ya katiba na sheria ili kuimarisha utawala bora na kuwawezesha wananchi kupata mafanikio makubwa ya kiuchumi na kufaidika na fursa za maendeleo.

Rais Samia alisema katika kipindi kifupi cha uongozi wake, Tanzania imepata mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali ikiwamo kimataifa ambapo diplomasia ya Tanzania nje ya nchi imeimarika.

Alisema kuimarika kwa siasa za nje kumeyafanya mataifa mbalimbali kuishika mkono Tanzania kwa kuiunga mkono katika harakati zake za kuimarisha uchumi na maendeleo.

Rais Samia alisema katika uongozi wake atahakikisha Tanzania inayafikiya malengo ya maendeleo endelevu yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa (UN) husu akisisitiza mwanamke hataachwa nyuma katika safari hiyo.

Alisema atahakikisha wanawake wananufaika na fursa mbalimbali zinazopatikana kwa ajili ya kuleta mabadiliko makubwa ya maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii.

Rais Samia pia alisema ameridhishwa na uongozi wa Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi ambaye ametimiza mwaka mmoja madarakani, akifanikisha mambo ya msingi aliyoyaahidi ikiwamo kupambana na rushwa na kuongeza kasi ya uwajibikaji serikalini.

Alisema katika kipindi chake amefanya kazi kubwa kuongeza kasi ya uwajibikaji huku akionyesha njia na dalili kwamba Tanzania bila rushwa inawezekana.

Rais Samia alisema Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni mfano wa kuleta umoja na utulivu ambao umewaunganisha wananchi wote na kuondosha siasa za chuki na uhasama.

Aliwataka Wazanzibar kuilinda serikali hiyo inayotokana na maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa ambayo yamefungua milango ya baraka ya kuelewana na kuondokana na siasa za chuki na mivutano.

Rais Samia pia aliwataka wanawake kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wakati wa uchaguzi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwakani.

Rais wa Zanzibar, Dk. Mwinyi alimshukuru Rais Samia kwa kumpa kila aina ya ushirikiano na misaada ikiwamo ya kiuchumi na maendeleo ambayo imekuwa chachu katika kuwainua wananchi.

Makamu Mwenyekiti wa UWT Zanzibar, Thuwaiba Kisasi, alisema wanawake wa Zanzibar kwa ujumla wanamuunga mkono na kumtakia kila la heri na mafanikio Rais Samia.

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali serikali na CCM, akiwamo Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na viongozi wastaafu wa UWT.

Habari Kubwa