Samia: Wekezeni kwenye madini

23Feb 2021
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
Samia: Wekezeni kwenye madini

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, kuwekeza kwenye sekta ya madini ambayo inakua kwa kasi nchini.

Amesema kuna haja wadau hao wa maendeleo ya uchumi kuwekeza katika sekta hiyo kwa kuwa Tanzania ni kati ya nchi zenye utajiri mkubwa wa madini aina mbalimbali, ikiwamo ya kipekee ya Tanzanite.

Samia aliyasema hayo jana, jijini Dar es Salaam, alipofungua Kongamano la Kimataifa la Madini na Uwekezaji 2021.

Alisema sekta hiyo imeendelea kuwa kinara nchini katika uingizaji mapato na mwaka jana iliongoza kwa ukuaji wa asilimia 17.7, huku ikiongoza kwenye mauzo ya bidhaa zenye thamani kubwa nje ya nchi.

Samia alisema sekta hiyo ni kati ya zinazovutia wawekezaji na kwamba Tanzania ni kati ya nchi tano Afrika zikiongoza kwenye uzalishaji madini.

Pamoja na kufanya vizuri huko, kiongozi huyo alisema kuna vikwazo vya uzalishaji na soko duniani, ikiwamo kusuasua kwa biashara ya madini.

Alisema sekta hiyo sasa inawainua wachimbaji madini tofauti na awali ambako kulikuwa na utoroshaji mkubwa na kufanya waliojiajiri kwenye sekta kubakia katika umaskini.

"Kufanyika kongamano hili na kukutanisha wadau wa sekta hii, ni jukwaa la kujulisha dunia kuhusu fursa tulizonazo za madini kuanzia uchimbaji, uchenjuaji na biashara.

"Ingawa ni kipindi kigumu katika dunia ikipitia janga la corona, ni wakati mgumu katika uchumi kwa mataifa mbalimbali. Nchi 24 zinashiriki kupitia mtandao kongamano hili," alisema.

Aliwataka washiriki wa kongamano kutumia fursa ya ushiriki kuibua kero na namna ya kuboresha sekta hiyo pamoja na kutumia fursa ya kibiashara.

"Tunawakaribisha mje kuwekeza, bado sehemu kubwa ya nchi ina hazina kubwa ya madini. Kupitia serikali, tunaweza kujenga ubia, tunaweza kufanya biashara ya madini pamoja.

"Tumeingia ubia na Barrick na sasa tuna Kampuni ya Twiga. Kampuni mbili zinakaribia kuungana nasi. Ni namna ya kutumia vizuri rasilimali zetu na kunufaika nazo, Tanzania si maskini," alisema.

Samia alisema kuwa hadi mwaka 2025, Sekta ya Madini itatoa mchango wa asilimia 10 na kwamba mwaka huu Wizara ya Madini imepangiwa kukusanya Sh. bilioni 526.7 na tayari zimeshakusanywa Sh. bilioni 360.74.

"Mjadili mambo ambayo yataendana na kufungamana na viwanda. Nchi nyingi za Afrika ikiwamo nchi yetu, zimechelewa kunufaika na rasilimali madini, tuchukue hatua madhubuti," aliagiza.

"Sasa, biashara inaimarika na hakuna malalamiko kutoka pande zote mbili. Tutashirikiana na wawekezaji wote kufanikisha ukuaji wa uchumi, tutaendelea kuboreshwa soko," aliongeza.

Alibainisha umuhimu wa wachimbaji madini wakubwa na wadogo kuzingatia sheria za nchi, kutoa ajira, kurejesha hisani kwa wananchi pamoja na kutunza mazingira kwa ustawi endelevu wa jamii.

Samia alisema kuna vikwazo kadhaa mbali na mafanikio, ikiwamo uhaba au kukosekana kwa nishati ya umeme kwenye maeneo ya uchimbaji na kuahidi utapatikanaji wake baada ya mradi mkubwa wa umeme utakaozalisha takribani megawati 4,000 utakapokamilika.

Awali, Waziri wa Madini, Doto Biteko, alisema kutokana na mafanikio kwenye raslimali madini, Tanzania imekuwa ikialikwa kushiriki mikutano ya kimataifa na kuamua kuanzisha kongamano kama hilo kufanyika nchini tangu mwaka 2019.

Alisema kongamano hilo linahudhuriwa na nchi kadhaa za nje zikiwamo zinazowakilishwa na mabalozi na mawaziri wa sekta hiyo, kujifunza na kubadilishana uzoefu.

"Sekta hii kwa asilimia 90 inaendeshwa na watu binafsi kwa kuwa wameamua kuwekeza fedha zao katika sekta hii. Serikali lazima tuwalee, kila aliyeweka pesa yake inarudi," alisema Biteko.

Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick, Mark Bristow, alisema ana imani kuwa fursa zipo kwa vijana wa kitanzania ambao watajiunga na kampuni hiyo.

Alisema migodi ni rasilimali za kitaifa na zinahitaji kuendeshwa kwa umakini, ikiwamo kutoa ajira na kuliingizia mapato taifa.

Alisema Dola za Marekani milioni 290 zilitumika katika uwekezaji wa kandarasi kwenye migodi yake ikiwamo Bulyanhulu na North Mara kwa mwaka jana.

"Utunzaji wa mazingira na usalama wa afya tunahakikisha wafanyakazi wanakuwa salama kila siku," alisema.

Habari Kubwa