Saruji ya Tanzania yapata soko EAC, SADC

15Aug 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Saruji ya Tanzania yapata soko EAC, SADC

TANZANIA imepata neema ya soko kubwa la saruji kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na zile za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, alisema hayo jana alipotembelea kiwanda cha kuzalisha saruji cha Camel, kilichoko Mbagala, jijini Dar es Salaam.

Bashungwa yuko kwenye ziara ya kukagua hali ya uzalishaji kwenye viwanda vya saruji kuangalia changamoto na kuzitatua baada ya nchi kadhaa kutaka kununua saruji ya Tanzania.

Alisema Tanzania ina viwanda 13 vya saruji ambavyo vina uwezo wa kuzalisha tani milioni 10.6 kwa mwaka lakini mahitaji ya ndani kwa mwaka yanafikia tani milioni sita tu, hivyo kuwa na uwezo wa kuzalisha ziada ya kuuza nje.

“Kwenye uzalishaji viwandani tuko vizuri sana na tunazidi kufanikiwa na ndiyo sababu wenzetu wameona nchini kwetu kuna fursa ya kununua saruji kwa sababu kwa sasa tuna ziada ya kuuza nje. Tunamshukuru Rais (John) Magufuli kwa maono yake makubwa kwenye sekta hii,” alisema.

Bashungwa alisema hatua ya nchi hizo kuiomba Tanzania izalishe saruji kwa wingi ili zije kununua ni jambo la kujivunia.

“Kutokana na fursa hii, Wizara tutaenda kila kiwanda kuangalia wanapokwama na tuwasaidie wasonge mbele kwasababu tukiongeza uzalishaji tutaongeza pia ajira kwa vijana wetu hapa nchini,” aliongeza Bashungwa.

Alisema kiwanda hicho kimejitahidi kuwekeza kwenye teknolojia ya kisasa na kuzalisha saruji nyingi na amewashauri watafute teknolojia zaidi kwaajili ya kujipanua zaidi ya Mbagala.

Waziri Bashungwa alisema serikali inataka kuona viwanda vya saruji vinajipanua na kujenga vingine kwenye mikoa ya kati na ile ya Kanda ya Ziwa ili kuachana na usafirishaji wa bidhaa hiyo kwa umbali mrefu.

Alimwagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Riziki Shemdoe, kukaa na wenye viwanda ili kuangalia wanavyoweza kuwekeza mikoa mingine na kama kutakuwa na changamoto wazitatue.

“Wizara inataka kujua mnataka nini na kwa sababu nia yetu ni kuona viwanda vinajengwa mikoa ya kanda ya kati na Kanda ya Ziwa tutawasaidia kutatua changamoto mtakazotuambia,” alisema.

Meneja Mkuu wa Camel Cement, Sundarraj Rajagopal, alisema wanaweza kuongeza uzalishaji kama watawekewa mazingira mazuri zaidi kama upatikanaji wa rasilimali za kuzalisha bidhaa hiyo.

Alisema serikali kupitia wizara hiyo itawasaidia sehemu ambayo wanaweza kupata kwa urahisi rasilimali ya ‘limestone’ na ‘crinker’ ili waongeze uzalishaji na bei ya bidhaa hiyo itashuka.

Habari Kubwa