Saudia yasaidia mashine 62 za kusafisha damu

18Jun 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Saudia yasaidia mashine 62 za kusafisha damu

SERIKALI imepokea msaada wa mashine za kusafisha damu 62 kutoka Saudi Arabia ambazo zitasambazwa mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar, ili kuondokana na changamoto ya wagonjwa kusafiri kwenda mikoa minne inayotoa huduma hiyo kwa sasa.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile (kushoto), akiangaliwa moja katika mashine 62 za kusafisha damu baada ya kukabidhiwa msaada na Naibu Balozi wa Saudi Arabia nchini, Ahmed Bin Saleh Alghamdi (wa pili kulia), jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Mratibu wa Magonjwa yasiyoambukiza wa wizara hiyo, Dk. Shadrack Buswelu. Habari Uk. 3. PICHA: GETRUDE MPEZYA

Msaada huo ulitolewa jana na Naibu Balozi wa Saudi Arabia nchini, Ahmed Bin Saleh Alghamdi, na kupokelewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile.

 

 

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo uliogharimu Sh. bilioni 1.5, huku mashine moja ikiuzwa Sh. milioni 25, Dk. Ndugulile alisema wagonjwa wamekuwa wakisafiri kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kwenda Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza na Kilimanjaro kwa ajili ya huduma hiyo.

Alisema msaada huo utasaidia wagonjwa badala ya kutumia muda mrefu kusafiri ili kuifikia mikoa hiyo inayotoa huduma hiyo kwa sasa, watapata kupitia mikoa yao.

“Tunaishukuru  Saudi Arabia kwa msaada huu  kwa sababu utasaidia katika sekta kutoa huduma kwa wagonjwa wenye uhitaji wa kusafisha damu, kwa sasa tuna vituo 19 ambavyo vinatoa huduma hii nchini, vingi vipo mkoa wa Dar es Salaam,” alisema.

“Kusudio la serikali ni kusogeza huduma hizi mikoani na tumeshaanza kujipanga kwa kuhakikisha tunatoa mafunzo ya wataalamu hao ili huduma ziweze kupatikana,” alisema.

Dk. Ndugulile alisema changamoto ya magonjwa yasiyoambukiza ni kubwa kwa sasa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa siku imekuwa ikifanya awamu tatu ya kusafisha damu.

“Tunafanya hivyo kuanzia siku ya Jumatatu hadi Jumamosi na mpaka Jumapili kwa siku za dharura tunaona wagonjwa kati ya 90 hadi 120 kwa siku.” alisema.

Mgonjwa wa figo anatakiwa kusafishwa mara mbili hadi mara tatu na Hospitali ya Muhimbili kuna awamu tatu kwa siku za kusafisha damu na zipo mashine 42.

Naye Naibu Balozi wa Saudi Arabia, Alghamdi, alisema nchi yao itaendelea kuisaidia Tanzania siyo tu kwa sekta ya afya na nyinginezo muhimu kama ya elimu.

Habari Kubwa