Saut yazindua dawati la unyanyasaji kijinsia

28May 2020
Rose Jacob
Mwanza
Nipashe
Saut yazindua dawati la unyanyasaji kijinsia

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, ameutaka uongozi wa Chuo Kikuu cha Saut, kuhakikisha dawati la kutatua changamoto za kijamii chuoni hapo halitumiki vibaya ili kuleta mstakabali ndani ya jamii.

Alitoa rai hiyo wakati akizindua dawati hilo, jana, katika chuo hicho kwa kushirikiana na Tahiliso.

Chuo hicho kimekuwa cha kwanza Tanzania kutekeleza agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alilolitoa Agosti 9, mwaka jana, la kutaka vyuo vyote nchini kuunda madawati ya kushughulikia changamoto vyuoni hasa unyanyasaji wa kijinsia.

"Suala la kutatua changamoto ndani ya vyuo na kijamii zinaihitaji weledi mkubwa ili kuleta usawa na kumaliza tatizo ili mambo yaende vizuri, na washauri mumtangulize Mungu katika kusikiliza mashauri hayo," alisema Mongella.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo cha Saut, Balozi Prof. Costa Mahalu, alisema kutokana na mwingiliano wa shughuli za kijamii ni vigumu kuzikwepa changamoto mbalimbali za kijamii kwa kiwango kikubwa zikiwamo watu kunyimwa haki ya kusikilizwa, unyanyasaji wa kijinsia, mikopo ya wanafunzi, migogoro na migongano, anuwai baina ya wanajamii.

"Tumeanzisha dawati hili ambalo litashughulikia matatizo mbalimbali ya wana Saut katika mahusiano yao hususani, wanafunzi kwa wanafunzi, wafunafunzi kwa wahadhiri, watoa huduma, watumishi wa utawala wa chuo, watumishi wa taasisi zilizopo ndani ya Saut, wanajamii wanaokizunguka chuo na nina imani chuo kufanikiwa," alisema Prof. Mahalu.

Habari Kubwa