SBL yafadhili masomo wanafunzi 10 Chuo Kilimo

17Feb 2020
Na Mwandishi Wetu
Moshi
Nipashe
SBL yafadhili masomo wanafunzi 10 Chuo Kilimo

WANAFUNZI 10 wanaosomea kilimo katika Chuo cha Kilacha Agriculture and Livestock Training Center, kilichoko Moshi mkoani Kilimanjaro, wamekuwa wa pili kunufaika na ufadhili wa msomo unaotolewa na Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) kwa wanafunzi wa kilimo nchini.

Chini ya mpango unaojulikana kama Kilimo-Viwanda, SBL inatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 50 kutoka katika jamii za wakulima kila mwaka kwa kuwalipia ada kwenye vyuo vya kilimo kwa kipindi chote cha masomo yao.

Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Mark Ocitti, akizungumza wakati wa hafla ya kutiliana saini katika Chuo cha Kilacha, alisema mpango huo unawalenga wanafunzi wanaotoka katika familia za wakulima ambazo hazina uwezo wa kuwalipia ada watoto wao na kuongeza kuwa itasaidia kuongeza wataalamu wa kilimo.

"Tunaamini kuwa mpango huu utawasaidia wanafunzi wanaotoka katika familia za wakulima zenye kipato cha chini kupata elimu ya juu huku pia ikichangia kuongeza wataalamu wa kilimo ambao watasaidia kuongeza uzalishaji," alisema.

Kwa mujibu wa Ocitti, mpango huo ni sehemu ya mkakati wa SBL wa kuongeza kiasi cha nafaka ambacho kampuni hiyo inanunua kwa ajili ya uzalishaji wa bia ambazo ni pamoja na mahindi, shayiri na mtama.

Alisema, mwaka jana SBL ilinunua zaidi ya tani za ujazo 17,000 za nafaka kutoka kwa wakulima wa ndani sawa na asilimia 70 ya mahitaji yake yote ya malighafi kwa mwaka.

"Kampuni ya SBL inalengo la kuongeza kiasi cha malighafi inayonunua kutoka kwa wakulima wa ndani hadi asilimia 85 kufikia mwaka 2020 na ndiyo maana tumeona umuhimu wa kusaidia kusomesha wataalamu wa kilimo ili wakafanye kazi ya kuboresha kilimo chetu. Kwa sasa kampuni inanunua malighafi kutoka kwenye mtandao wenye wakulima 400 hapa nchini," alisema.

Kwa upande wa mkuu wa kituo hicho, Benito Mwenda, aliishukuru SBL kwa ufadhili alioutoa na kuzitaka taasisi binafsi kujitokeza na kusaidia sekta ya kilimo ambayo ni sekta mama.

Mwezi Januari, Chuo cha Kaole Wazazi College of Agriculture kilichopo Bagamoyo mkoani Pwani, kilikuwa ni cha kwanza kunufaika na mpango huo wa ufadhili wa masomo unaolenga kuongeza wataalamu katika sekta ya kilimo nchini.

Habari Kubwa