Scorpion afungwa miaka 7 kumtoboa macho mtu

23Jan 2018
Elizaberth Zaya
Nipashe
Scorpion afungwa miaka 7 kumtoboa macho mtu

MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, jana ilimhukumu Salum Njwete, maarufu kama Scorpion, kutumikia kifungo cha miaka saba jela na kulipa faini ya Sh. milioni 30, baada ya kupatikana na hatia ya kujeruhi mwili ikiwamo kumtoboa macho, Said Mrisho.

Scorpion (36), ni mwalimu wa sanaa ya kujihami. 

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Flora Haule, huku upande wa Serikali ukiongozwa na Frank Tawale na upande wa utetezi ukiwa na wakili Hussein Hitu.

Akisoma huku hiyo, Hakimu Flora alisema mtuhumiwa alikuwa anashtakiwa kwa makosa mawili la unyang'anyi wa kutumia silaha na kujeruhi mwili.

Hakimu alisema upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha dhidi ya mtuhumiwa huyo, hivyo kukutwa na hatia katika kosa moja la kujeruhi.

Hakimu Haule alisema kuwa upande wa mashtaka ulileta mashahidi 10 na mshtakiwa alijitetea mwenyewe.

Alisema mshtakiwa alikutwa na hatia kupitia kifungu namba 225 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Hakimu Haule alisema mahakama imejiridhisha kuwa mlalamikaji Said Mrisho alishambuliwa kutokana na majeraha mbalimbali ambayo madaktari walithibitisha kwenye mwili wake.

"Mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa kwamba mshtakiwa ndiye aliyemjeruhi mlalamikaji kinyume na sheria hata kama alikuwa na makosa," alidai Hakimu Flora.

"Ushahidi umeonyesha kuwa Scorpion alikuwa anajishughulisha na ulinzi na hata uhalifu eneo la Buguruni umepungua kwa kazi yake," alisema Hakimu Haule.

Hakimu alisema utetezi wa mshtakiwa ulionyesha kuwa dhamira yake ilikuwa kupambana na mtu aliyemdhania kuwa ni mhalifu na haikuwa nia yake kuiba.

Pia alisema katika ushahidi uliotolewa hakuna shahidi aliyeeleza kama mshtakiwa aliiba.

Kabla ya kutolewa adhabu, Wakili wa Serikali, Tawale aliiomba mahakama kutoa adhabu stahiki kwa mshtakiwa kwa kuzingatia ulemavu aliosababishiwa mlalamikaji.

Tawale alisema taifa limepoteza nguvu kazi kwa mlalamikaji kupata ulemavu na kwamba pamoja na kwamba alikuwa anategemewa na familia yake, kutokana na madhara aliyoyapata hawezi kuwajibika tena na ndoto zake zimefifia.

Akitoa utetezi, wakili Hitu aliiomba mahakama impunguzie adhabu mshtakiwa kwa kuwa ni kosa lake la kwanza na ni mtu mwema kwa kuwa hata ushahidi umeeleza kuwa amesaidia kupunguza uhalifu eneo la Buguruni, Manispaa ya Ilala.

Hitu alisema mshtakiwa ana familia inayomtegemea na hivyo kwa sababu hawezi tena kuihudumia ni vema Mahakama ikatenda haki kwa kutoa adhabu inayoendana na kitendo alichofanyiwa. 

Hakimu Haule alisema mshtakiwa atatakiwa kulipa fidia ya Sh. milioni 30 kwa haraka kama fidia ya madhara yaliyopatikana kwa mlalamikaji.

Katika kesi ya msingi ilidaiwa kuwa Septemba 6, 2016 huko Buguruni eneo la Sheli, mshtakiwa Njwete alimchoma Mrisho kwa kisu katika sehemu mbalimbali za mwili wake, ikiwamo katika macho, tumbo na mabegani na kumsababishia majeraha makubwa.

Aidha, ilidaiwa baada ya kutekeleza shambulizi hilo, Scorpion aliiba cheni ya madini ya fedha gramu 38 yenye thamani Sh. 60,000, bangili ya mkononi na Sh. 331,000 pamoja na pochi vyote vyenye thamani Sh. 476,000, mali ya Mrisho.

Habari Kubwa