Sekondari wanolewa uombaji mikopo HESLB

15Apr 2019
Na Mwandishi Wetu
Simiyu
Nipashe
Sekondari wanolewa uombaji mikopo HESLB

 
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeanza kuendesha programu za elimu kwa wanafunzi wa shule za sekondari waliopo mikoani ili kuwaelimisha kuhusu sifa na taratibu za kuomba mikopo kwa usahihi.

Akizungumza wilayani Maswa, mkoani Simiyu na wanafunzi 1,166 wa kidato cha sita kutoka shule zote 12 za mkoa huo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, alisema uendeshaji wa programu hizo unalenga kuondokana na changamoto wanazopata wanafunzi wakati wa kuomba mikopo ya elimu ya juu.

HESLB ilianza kuendesha programu hizo katika mkoa wa Dar es Salaam.
 
Wanafunzi hao wapo katika kambi iliyoandaliwa na uongozi wa mkoa wa Simiyu kwa ajili ya maandalizi ya mitihani ya kidato cha sita inayotarajiwa kufanyika mwezi ujao wa Mei. Kambi hiyo ipo katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa.
 
“Uzoefu wetu na maoni ya wadau wetu umetufanya tuanzishe programu hizi nchini kote ili wakati wa kuomba mikopo, muombe kwa usahihi na wale wenye sifa wapate na hatimaye kutimiza ndoto zao,” aliwaambia wanafunzi hao na kueleza kuwa kuanzia kesho (Aprili 15, 2019) maofisa wa HESLB watakuwa katika shule mbalimbali mikoani kutoa elimu hiyo,” alisema.
 
Katika mikutano hiyo, wanafunzi wanaelezwa kuhusu sifa, nyaraka muhimu zinazotakiwa, namna ya kuomba na kuwasilisha kwa usahihi kwa njia ya mtandao na utaratibu na umuhimu wa kurejesha mkopo mara wamalizapo masomo. Katika programu hizi, wanafunzi pia hupata fursa ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi.
 
Kwa mujibu wa Badru, katika mwaka wa masomo 2018/2019, kati ya waombaji wa mikopo zaidi ya 57,000 ambao walipata udahili vyuoni, maombi zaidi ya 9,000 yalikuwa na upungufu mkubwa ikiwamo kukosa nyaraka kama vyeti vya kuzaliwa, vitambulisho sahihi vya wadhamini, kutosainiwa na waombaji, wadhamini au serikali za mitaa au vijiji.
 
Ofisa Mikopo Mwandamizi kutoka HESLB, Daudi Elisha, aliwasihi wanafunzi hao kusoma kwa makini mwongozo utakaotolewa na HESLB mwezi ujao ambao utaeleza hatua kwa hatua kuhusu uombaji wa mkopo.

Habari Kubwa