Sekondari yasaidiwa vyakula

14Feb 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Sekondari yasaidiwa vyakula

TAASISI ya Humanity First Tanzania imetoa msaada wa vyakula vyenye thamani ya Sh. milioni 5 kwa ajili ya wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Idifu Wilaya ya Chamwino, mkoa wa Dodoma kwa nia ya kukabiliana na njaa iliyoikumba.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo kwa niaba ya mkurugenzi mkuu wa taasisi hiyo, Sheikh wa Kanda ya Kati wa Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya, Bashart Ur Rehman Butt, alisema msaada huo umetolewa na taasisi hiyo ili wanafunzi hao wazingatie masomo yao vizuri kwani hilo ni vigumu kuwezekana ikiwa wataendelea kukabiliwa na njaa.

“Tulivyopata taarifa ya kuwapo kwa changamoto ya njaa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kupitia Mwenyekiti wa Halmashauri, tuliguswa sana baada ya kusikia kuwa mahudhurio ya wanafunzi wa shule hiyo yameshuka kutokana na tatizo la chakula... tunaamini kiasi hiki kitasaidia,” alisema Butt.

Mwanafunzi Flora Mamuli, akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, alisema kuwa kupatikana kwa msaada huo kutawawezesha kusoma kwa umakini zaidi tofauti na awali ambapo wengi wao walikuwa wakitoroka kurudi nyumbani kabla ya muda wa vipindi vya masomo kumalizika kutokana na njaa.

“Jumla yetu hapa tupo wanafunzi 250. Kuna wakati hata kunywa uji asubuhi hapa shuleni tulishindwa, lakini hivi sasa tuna uhakika wa kusoma kwa bidii na mahudhurio yataongezeka kama zamani,”alisema.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Musa Kaweya, ambaye pia ni diwani wa kata hiyo, alisema kuwa tatizo la njaa katika wilaya hiyo limesababisha kushuka kwa idadi ya mahudhurio kutokana na wanafunzi wengi kuwa watoro.

“Ni imani yangu kuwa kwa wale wote waliokuwa mahudhurio yao siyo ya kuridhisha, sasa watahudhuria masomo vizuri kwa kuwa kutakuwepo uhakika wa walau kunywa uji asubihi na pia chakula cha mchana kwa wanafunzi wote wa shule hii,” alisema.

Habari Kubwa