Sekta binafsi yatoa neno ujenzi wa miundombinu

20Oct 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Sekta binafsi yatoa neno ujenzi wa miundombinu

WADAU wa Sekta Binafsi wamepongeza ujenzi wa miundombinu ikiwemo reli ya kisasa (SGR) na bwawa la ufuaji umeme vitasaidia kuchochea fursa za uwekezaji hususani kwenye viwanda kwenye maeneo mbalimbali.

Mwenyekiti wa TPSF, Angelina Ngalalu.

Akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Taasisi na Taasisi ya Sekta Binafsi hapa nchini (TPSF),kwa lengo la kuipongeza serikali kwa mchango wake mkubwa wa kuinua sekta binafs jijini Dar es Salaam juzi, Mwenyekiti wa Taasisi ya sekta hiyo, Angelina Ngalalu, alisema ujenzi wa miundombinu ni miongoni mwa mafanikio makubwa katika kuinua uchumi wa taifa.

”Kwa miaka mitano Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli imefanya makubwa sana na yenye tija kwa uchumi wa Taifa, tunaamini kama wawekezaji tutatumia kila fursa inayopatikana kufanya uwekezaji kulingana na mazingira mazuri yaliyowekwa na serikali,’’ alisema Ngalula.

Alisema kuwa ujenzi wa reli ya kisasa na miundombinu mingine kama bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 utaongeza soko la ajira kwa vijana wa Kitanzania na hivyo kuchangia ukuaji wa pato la taifa.

“Katika kipindi cha miaka mitano tumeshuhudia ujenzi wa miundombinu ya kimkakati ambayo imechangia upatikanaji wa ajira kwa vijana wa Kitanzania na ajira zaidi zitakuja punde ujenzi wa miundombinu hiyo utakapokamilika kwa kuwa wadau wa sekta binafsi watawekeza katika miundombinu hiyo,” alisema.

Alisema ujenzi wa reli hiyo utaongeza kiwango cha mizigo itakayosafirishwa kutoka tani milioni tano kwa mwaka kwa sasa na kufikia tani milioni 14 kwa mwaka.

‘’Ujenzi wa SGR utasaidia kuongeza kiwango cha mizigo

itakayosafirishwa kutoka tani milioni tano kwa mwaka kwa sasa hadi tani milioni 14 kwa mwaka pindi ujenzi utakapokamilika,’’ alisema na kuongeza kuwa hali hiyo itaongeza tija kwenye uchumi na ukuaji wa biashara kwa nchi.

Aidha ameiomba serikali kuendelea kutoa ushirikiano kwa Taasisi hiyo kama ambavyo imefanya kwa kipindi chote cha miaka mitano ili kujenga uchumi imara na wenye kuleta tija kwa wananchi.

“Katika nchi nyingi zilizoendelea zilifanya hivyo kwa kuweka mazingira rafiki ili wadau wa sekta binafsi waweze kufanya uwekezaji.”

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha bodaboda nchini, Michael Haule,  alisema kupitia vikundi vyao wamepata bima ya afya kwa gharama nafuu.

Habari Kubwa