Sendiga kumpa JPM uwaziri

19Oct 2020
Francis Godwin
Iringa
Nipashe
Sendiga kumpa JPM uwaziri

MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Queen Sendiga, amesema akichaguliwa kuwa Rais wa Tanzania, akiunda baraza la mawaziri atampa nafasi Rais John Magufuli, kuwa waziri wa ujenzi.

Aidha, baada ya kuapishwa atafanya maboresho makubwa katika sekta ya afya kwa huduma za ngazi za chini kuboreshwa kwa kuwa na zahanati za kisasa kila kijiji.

Akiomba kura kwa wananchi wa Iringa mjini jana, alisema mtu pekee mwenye uwezo wa kusimamia sekta ya ujenzi ni mgombea Dk. Magufuli kutokana na kuimudu vyema sekta hiyo alivyokuwa Waziri katika serikali zilizopita.

Alisema pia atahakikisha wagombea urais wote waliojitokeza kuwania nafasi hizo wanapata nafasi za uongozi ndani ya serikali yake kulingana na sifa na uwezi wao.

Sendiga alisema ameamua hivyo kutokana na ukweli kuwa chama chake hakina wagombea ubunge wa kutosha nchini na kwamba itakuwa vigumu kupata mawaziri wa kutosha ndiyo maana lazima achukue wagombea urais ambao tayari wameonesha uwezo wao .

Alisema kuwa katika mchakato wa kampeni unaoendelea mbali ya kufanikiwa kupita mikoa zaidi ya 15 hadi sasa, ila amefuatilia kampeni za wagombea wenzake na sera zao na sehemu kubwa anajua ni yupi atamchukua katika serikali yake kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania.

Kwa mujibu wa mgombea huyo, bado kuna changamoto kubwa katika uboreshaji wa sekta ya afya kwa kuwa na zanahati kila kijiji kwake ni kipaumbele maana wananchi wanapata kero kubwa sana ya huduma za afya vijijini na uboreshaji huo utakwenda sambamba na vifaa tiba zikiwemo dawa .

Alisema kuwa hali ya uchumi siyo nzuri miongoni mwa Watanzania pamoja na serikali kujinasibu kuwa uchumi umekua ila uchumi huo hauwalengi moja kwa moja wananchi kuwa na fedha katika mifuko yao ambapo ADC watahakikisha wanatumia rasilimali zilizopo kukuza uchumi .

“Jukumu lingine kubwa kwa Serikali makini inayojali maisha ya watu ni kupanga namna njema ya matumizi ya rasilimali zilizopo kwenye maeneo husika kwa manufaa ya wakazi wake.

Aidha, alisema akiwa raia atarejesha ujenzi wa kiwanda cha gesi Mtwara kama namna ya kurejesha matumaini kwa wananchi wa kusini na kwamba serikali yake haitawakopa mazao wananchi na badala yake itawatengenezea mfumo wa kuwalipa kabla ya kuchukua mazao yao .

Habari Kubwa