Serikali kuikabidhi NSSF bwawa Kidunda 

23Jan 2018
Frank Monyo
Nipashe
Serikali kuikabidhi NSSF bwawa Kidunda 

SERIKALI inafikiria kufanya mazungumzo na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), ili kulikabidhi mradi wa ujenzi wa bwawa la Kidunda lililoko mkoani Morogoro.

Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Maji, Mifugo na Kilimo, Daniel Nsanzugwanko, (katikati) akizunguzma jambo na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Romanus Mwangi’ngo, (kushoto) na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo emmanuel Papian, walipotembelea mtambo wa maji wa Ruvu Juu, Mlandizi mkoani Pwani.

Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam, Romanus Mwang’ingo, alisema lengo la serikali ni kuiwezesha Dawasa kuondoka na utegemezi wa maji ya mvua katika vyanzo vyake vya Ruvu Chini na Ruvu Juu.

Mwang’ingo alibainisha hilo mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akizungumza mbele ya  Kamati ya Bunge ya Maji, Mifugo na Kilimo.

Mtendaji mkuu huyo, alikuwa akiwasilisha ripoti ya uendeshaji wa miradi mbalimbali kabla ya kuanza ziara ya kamati kutembelea na kukagua miradi inayotekelezwa na kusimamiwa na Dawasa na Shirika la Dawasco, iliyopo Dar es Salaam na Pwani.

Mwang'ingo alisema mradi huo ni wa siku nyingi na ulisanifiwa miaka mitatu iliyopita.

Alisema kwa sasa zinatafutwa fedha ambazo zitakuwa za masharti nafuu kutekeleza mradi huo na katika kufanikisha hilo, serikali iko katika mazungumzo na NSSF, ili ikabidhiwe kama ilivyojenga Daraja la Kigamboni.

Ujenzi wa bwawa hilo utasaidia mitambo ya kuzalisha maji ya Ruvu Chini na Ruvu Juu ambayo inategemea maji kutoka Mto Ruvu ambao chanzo chake ni maji ya mvua, Mwang'ingo alisema.

Wakati wa kiangazi uzalishaji maji na usambazaji huwa mdogo jijini Dar es Salaam.

"Serikali ilikuwa inafikiria mradi huu kutekelezwa na NSSF kama ule wa ujenzi wa Daraja la Kigamboni kwa gharama nafuu na baadaye uweze kujiendesha wenyewe," Mwang'ingo alisema.

"Utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme na tutakuwa na uwezo wa kutumia maji hayo kwa miaka 30 ijayo."

Baada ya kutembelea miradi hiyo, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Emmanuel Papian, alisema kazi iliyofanyika ni kubwa na wameona jinsi gani fedha za serikali zimetumika ipasavyo katika kuhudumia wananchi katika sekta ya maji.

Papian alishauri umakini uwepo pale wanapotafutwa makandarasi wa kuendesha miradi hiyo kwani miradi mingi inatekelezwa kwa fedha za mkopo kutoka India na kila kitu kinafanywa na kampuni kutoka India, jambo ambalo sio sahihi.

"Inawezekana kuna mahali ambapo tumezidiwa au kujichanganya wenyewe na kama ni kwenye makubaliano ya huo mkopo inapaswa tuangalie upya ili kuweka mamba sawa," alisema mwenyekiti huyo.

"Kamati inashauri watendaji wa ndani wanapomaliza hii miradi basi vijana wa Kitanzania lazima wawe wameshajua na kufundishwa na wajifunze kila kitu ili waweze kuendesha miradi hii kikamilifu hapo baadaye."

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Dawasa, Laston  Msongole, alisema nia ya mamlaka ni kuhakikisha maeneo yote ambayo hayajafikiwa na huduma ya maji hususan wilaya mpya ya Kigamboni, yanafikiwa na huduma hiyo. 

BILIONI 7.4/-Serikali imeshalipa fidia ya Sh. bilioni 7.4 kwa familia 2,603 kupisha ujenzi wa Bwawa la Kidunda lililopo katika kata ya Serembala Kiganila. 

Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji wakati huo, Isaack Kamwelwe aliliambia Bunge Mei 13, mwaka jana kuwa Serikali ilitenga Sh. bilioni 1.5 kwa mwaka wa fedha 2016/2017 na ilipanga kutenga Sh. bilioni mbili kwa mwaka wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya fidia kulingana na tathmini iliyofanywa.

“Serikali inaandaa malipo ya fidia kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 ambayo inaelekeza pia kuwa endapo malipo ya fidia yatachelewa kulipwa kwa zaidi ya miezi sita tangu kupitishwa, mlipaji atapaswa kufanya mapitio na kulipa nyongeza na muda uliozidi,” alisema.

Kamwelwe alikuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Prosper Mbena(CCM) aliyetaka kufahamu kama serikali iko tayari kuboresha malipo ya fidia kwa wanavijiji wote walioathirika kwa nyumba na mashamba yao kuchukuliwa kupisha ujenzi wa Bwawa la Kidunda na kama serikali iko tayari kwenye bajeti hii kumalizia malipo ya takribani Sh. bilioni 3.7 kuwafidia wananchi hao, kulingana na tathmini iliyofanyika. 

Habari Kubwa