Serikali, mabalozi wateta kuhusu sakata la Loliondo  

21Jun 2022
Halfani Chusi
DAR ES SALAAM
Nipashe
Serikali, mabalozi wateta kuhusu sakata la Loliondo  

SERIKALI imekutana na mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao nchini pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa kujadili mustakabali wa kinachoendelea Loliondo na Ngorongoro.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula.

Jijini Dar es Salam leo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, alipokutana na wadau hao katika kikao hicho maalum, alikanusha uvumi ulioenea ukidai serikali imetumia nguvu na kukiuka haki za binadamu katika kuwahamisha baadhi ya wakazi walioko maeneo hayo.

Amesema taarifa hizo siyo za kweli na zinapaswa kupuuzwa huku akibainisha kuwa serikali imetenga maeneo maalum kwa ajili yao na mtu atahamia kwa hiari yake mwenyewe kutokana na kuvutiwa na huduma zilizowekwa na serikali.

Balozi Mulamula amesema kikao hicho kilikuwa mahususi kwa kutoa sintofahamu kwa baadhi ya mabalozi, wadau wa mashirika ya kitaifa na wananchi wengine kuhusu kinachotajwa kuwa mgogoro kuhusu Loliondo na Ngorongoro.

"Katika vikao vyetu hivi vya kupashana habari, tumekuwa pia tukiwaalika mawaziri wa sekta hizo. Kumekuwa na taarifa mbalimbali zikisambaa zikidai Loliondo na Ngorongoro wananchi wanaondolewa kwa nguvu na kwa kukiuka haki za binadamu.

"Kwa hiyo, leo ninadhani ufafanuzi uliotolewa na Naibu Waziri (Mary Masanja) pamoja na Mkurugenzi wa Wanyamapori katika wasilisho hili limeondoa sintofahamu kwenye vichwa vya watu," amesema.

Kwa hiyo kinachoendelea Loliondo siyo kuhamisha watu kwamba sasa kumewekwa mipaka upande mmoja kwa ajili ya wanyama na uhifadhi lakini eneo lingine ni kwa ajili ya wananchi na zaidi Km 2,500 zimeachwa kwa ajili yao.

"Kwa hiyo, hakuna anayeondolewa, wanaoondoka ni wa kutoka Ngorongoro kwa sababu kule watu wamepoteza watoto wao, watu wanaliwa na wanyama wakali. 

"Kwa hiyo, serikali baada ya kuliona hilo, imekuja na mkakati kabambe wa kuwatafutia maeneo mengine na kuwapatia mazingira mazuri yenye huduma nyingi za kijamii na wamepewa zaidi ya ekari tano kwa wote wanaohamia Loliondo na baadhi ya wakazi zaidi ya 200 wameshaanza kuhamia huko," amefanua.

Amesema kuwa hali iko shwari licha ya askari mmoja kuuawa wakati wa kutetea amani lakini hakuna anayelisemea hilo, akibainisha kuwa taarifa ya serikali imepokewa kwa furaha na mabalozi kutokana na kuwa na ufafanuzi mzuri.

"Hakuna anayeshurutishwa kuondoka, hakuna anayeondolewa kwa nguvu. Wanaondoka kwa hiari lakini wakiona faida kule, wanakohamia kuna huduma nzuri wataenda wenyewe.

"Kwa hiyo, sisi kama wizara tumetaka jumuiya ya kimataifa, mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao pamoja na wananchi wengine, waelewe kwa ufasaha zaidi kile kinachoendelea dhidi ya sakata hilo," amesisitiza.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja, amesema kumakuwapo na uvunjifu wa sheria kwa baadhi ya wakazi wanaoishi maeneo hayo, hali iliyopelekea serikali kuwatafutia njia nyingine ya kuishi.

Amesema sheria iliyowekwa kwa wananchi wanaishi Ngorongoro haimruhusu mkazi kufanya shughuli nyingine za kujamii zaidi ya kufuga tu.

"Ni kula tu, tukasema hapana, sasa tuwaelimishe hawa watu kama unataka kufanya biashara, kama unataka kuendesha pikipiki, kujenga ghorofa, tutoe eneo maalum ambalo litakuwa hiari mtu kutoka katika maisha hayo kwenda katika maisha mengine kwa sababu kama binadamu anapaswa kuishi vizuri.

"Kwa hiyo, tukasema kwetu sisi kama kweli Watanzania tunaangalia haki za binadamu, kuna haja ya kuwasaidia hawa watu kwa sababu wengine wanateseka na wengine wapo katika hatari ya kuliwa na wanyama wakali kama vile simba," amesema.

Mmoja wa wakazi wa Ngorongoro, Jumanne Jafari, alipiga simu katika mkutano huo wa na kukiri kuwapo kwa hatua hizo na baadhi ya watu wameanza kuhama Loliondo na wengine wanajiandaa kuhamia kwenye makazi mapya yaliyoandaliwa na serikali mkoani Tanga.

Habari Kubwa