Serikali Shinyanga yakanusha kulemewa wagonjwa wa corona

12Jul 2021
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
Serikali Shinyanga yakanusha kulemewa wagonjwa wa corona

SERIKALI mkoani Shinyanga, imekanusha taarifa ambazo imedai ni za uongo zilizosambazwa na Mwenyekiti wa BAVICHA mkoani Iringa, Vitusi Nkuna kupitia mitandao ya kijamii, kuwa mkoa huo umelemewa na wagonjwa wa corona,na ina uhaba wa Mitungi ya Oksijeni.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk, Philemon Sengati, akizungumza kwenye Hospitali ya Rufaa mkoani humo kuwa hakuna idadi kubwa ya wagonjwa wa Corona kama ilivyozushwa kwenye mitandao ya kijamii.

Mkuu wa mkoa huo Dk. Philemoni Sengati, amekanusha taarifa hizo leo wakati akizungumza na watumishi wa Serikali, na alipo watembelea wagonjwa wa corona ambao wamelazwa katika Hospitali ya Rufani mkoani humo.

Amesema baada ya kuona tarifa hizo mtandaoni ambazo zimezua taharuki, ndipo akaona ni vyema atembelee pia katika hospitali hiyo ili kujionea mwenyewe hali halisi, na kukuta hakuna idadi ya wagonjwa wengi kama ilivyo enezwa kwenye mitandao ya kijamii.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk. Philemon Sengati, kulia, akizungumza na baadhi ya wagonjwa wa Corona ambao wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa mkoani humo.

“Serikali ya Mkoa wa Shinyanga, tumesikitishwa sana na taarifa hizi ambazo zime enezwa kwenye mitandao ya kijamii na Mwenyekiti wa BAVICHA mkoani Iringa Vitus Nkuna, kuwa tumelemewa na wagonjwa wa corona na hatuna Mitungi ya Oksijeni kitu ambacho ni uongo,”amesema Dk.Sengati na kuongeza;

“Mwenyekiti huyu wa BAVICHA lazima Serikali tumchukulie hatua kali za kisheria kwa kuzusha uongo na kuleta taharuki kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga, hatukatai wagonjwa ni kweli wapo, lakini siyo wengi kama inavyoenezwa na wanaendelea kupata matibabu,”ameongeza.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk, Philemon Sengati, akinawa mikono katika Stand ya Mabasi mjini humo, alipowasili kutoa elimu ya corona.

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa mkoa, akiwa katika Standi ya Mabasi ya kwenda wilayani, amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa corona, kwa kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka, kuvaa barakoa, kupaka vitakasa mikono, pamoja na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk. Yudas Ndugile, amewataka wananchi pale wanaposikia dalili za ugonjwa huo, wawahi kwenye huduma za afya, huku akitaja vituo ambavyo vimetengwa kwa ajili ya kutoa huduma hiyo, kuwa ni Hospitali ya Rufaa, Kolandoto, kituo cha afya Kambarage.

Dk. Ndugile ametaja vituo vingine kuwa ni Kituo cha afya Tinde, Bugharama, Nyamilangano, Hospitali ya Iselamagazi wilayani Shinyanga. pamoja na Hospitali ya wilaya ya Kahama, huku akitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni kuchoka, kusikia homa, viungo kuuma, kushindwa kupumua vizuri, na kuharisha.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk, Philemon Sengati, akitoa elimu ya corona katika Stand ya Mabasi mjini humo.