Serikali yalipongeza Jukwaa la Misitu Afrika

13Dec 2021
Salome Kitomari
Nipashe
Serikali yalipongeza Jukwaa la Misitu Afrika

SERIKALI imesema inatambua kazi kubwa inayofanywa na Jukwa la Misitu Afrika (AFF), kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuelimisha jamii juu ya nafasi ya misitu kwenye mabadiliko ya tabia nchi, namna ya kukabili na kupunguza hali hiyo huku maisha ya watu na viumbe yakiendelea.

Wataalam wa misitu kutoka nchi mbalimbali wakimsikiliza Meneja wa Msitu unatunzwa na Chuo Kikuu cha Sokoine,Morogoro (SUA).mkoani Arusha

Hayo yalisemwa hivi karibuni na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo, wakati akifungua mafunzo ya misitu kwa wataalam wa sekta hiyo kutoka nchi za Burkna Faso, Nigeria, Kenya, Malawi, Ethiopia, Msumbiji, Cameroon, Zamba na Zimbabwe.

 

Katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Chuo cha Misitu, Wanyamapori na Utalii cha Chuo Kikuu cha Kilimo SUA, Prof. Suzana Augustino, alisema mchango wa msitu kwenye mabadiliko ya tabia nchi ni mkubwa na unapaswa kutambuliwa kwa kuwa una msaada mkubwa.

 

Aidha, aliwapongeza AFF kwa mchango muhimu kwenye maendeleo ya misitu barani Afrika kupitia mfumo wake wa usimamizi wa sera ya sayansi, ambao umekuwa na manufaa kwa maendeleo na mchakato wa maamuzi kuhusu misitu kwenye nchi mbalimbali.

 

Kwa mujibu wa Prof. Silayo, kwa miongo kadhaa masuala ya mazingira ya kimataifa yenye umuhimu mkubwa kwenye misitu barani Afrika yameibuka ambayo ni mabadiliko ya tabia nchi, uharibifu wa ardhi, malengo ya maendeleo endelevu na uchumi wa kijani ambayo ni fursa  ya kuhakikisha misitu inazidi kutunzwa kwa faida vizazi vyote ni muhimu.

 

Alisema kuna fursa nyingi zilizoletwa na mabadiliko ya tabia nchi kwenye sekta ya misitu ambayo inahitaji kujenga uwezo wa kuelezea na kuziunganisha na utekelezaji wa mipango ya kimataifa, Agenda ya Umoja wa Afrika 2023 na mipango ya maendeleo ya nchi.

 

“Utayari wa serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), sekta binafsi na jamii unahitaji uelewa wa kutosha kwenye hatua zinazozchukuliwa, AFF imekuwa mstari wa mbele kuwajengewa uwezo wanachama wa mtandao ambao ni wataalam wa misitu ambao wamekuwa na mawazo chanya na ya kina kuhusu misitu na mabadiliko ya tabia nchi,”alisema.

Alisema licha ya utayari wa kimataifa unaonekana kwenye suala la mabadiliko ya tabia nchi lakini serikali zinatambua wajibu wa raslimali misitu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa watu na misitu yenyewe na kwamba AFF walifanya uchambuzi wa kina wa nafasi ya misitu ya Afrika kukabili mabadiliko ya tabia nchi na kuwasaidia watu kuwa na elimu na namna ya kufanya shughuli zao za kuboresha masiha yao, viumbe hai na utunzaji wa mazingira.

 

Awali, Katibu Mtendaji wa AFF, Prof, Godwin Kowero, alisema Jukwaa hilo lilianzishwa mwaka 2006/07 na liliona changamoto zilizopo zitatatulika lakini mazingira yamebadilika na sasa kuna ongezeko la jaoto na changamoto zake ambavyo vinaumiza vichwa vya wanataalam duniani.

 

Alisema misitu na miti, aridhi, vyanzo vya maji, bahari na tekonolojia iliyobaoreshwa vinaonekana ndiyo vitaokoa jamii kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa kuangalia maisha ya viumbe hai na mimea.

Kwa mujibu wa Prof. Kowero, kukosekana kwa majisafi na salama ni tatizo kubwa kwa sasa linalotishia uhai wa binadamu, wanyama na viumbe wengine wanaoishi ardhini na linahitaji nguvu ya pamoja kupunguza athari.

 

“Mara kadhaa tunasikia watu wamekufa kwa kiu ya maji lakini ongezeko la migogoro baina ya wanyama na bianadamu wengi ni wakulima wadogo ambao wana nafasi kubwa na hapa ndiyo tunaona misitu na miti kama suluhisho la matatizo haya,”alisema.

Naye, Prof, Suzana ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la AFF, alisema ni lazima nchi ziipe kipaumbele agenda ya msitu kwa kuwa siyo kawaida mvua kuchelewa kama sasa na kwamba athari ni kubwa kwa wanyama na biandamu.

 

“Ukienda kwa wakulima hali ni mbaya mazao hayajaota na yaliyoota yamekauaka, mifugo inakufa na bei imeshuka kiasi kwamba hawaoni faida huku mingine ikifa, misitu ni muhimu sana katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi,”alisema

Habari Kubwa