Serikali yaonya wataalamu wa afya kutoa chanjo kiundugu

03Aug 2021
Mary Mosha
Moshi
Nipashe
Serikali yaonya wataalamu wa afya kutoa chanjo kiundugu

​​​​​​​SERIKALI mkoani Kilimanjaro imesema haitamvumlia mtaalamu yeyote  wa idara ya afya mkoani hapo, atakayetoa chanjo kwa upendeleo na badala yake amewataka kuwasaidia wahusika kwa kuwapa maelekezo sahihi katika ujazaji wa fomu hasa kwa wasio tumia simu janja (smartphone).

Hayo yamesemwa leo na Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Moshi Saidi Mtanda, wakati wa uzinduzi wa chanjo Uviko 19, amesema hawatamvumilia mtaalamu yeyote atakyependelea ndugu, jamaa na marafiki zake katika utoaji wa huduma.

“Leo tunazindua zoezi hili katika kituo cha afya Majengo, lakini  tutatembelea na  kujionea hali ya utoaji wa huduma katika hospitali ya rufaa ya Mawenzi,  hospitali ya Rufaa ya kanda  KCMC na kituo cha afya cha Pasua. Matatizo madogo madogo hayakosekani, ila tunayafanyia kazi katika kuakikisha zoezi hili linaendelea vizuri na kwa wakati,”

"Hatutegemei wataalamu wetu kutumia mwanya huo, kupokea rushwa  kwa kuwalaghai  wananchi watoe ili waweze kufanyiwa kwa haraka zaidi, tukikugundua hatutakuacha,  nyinyi zingatieni  wazee wapate huduma kwanza kama sera ya afya inavyoelekeza pamoja na  watu wenye magonjwa sugu,” amesema Mtanda.

Aidha, mewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupata chanjo hiyo huku akiwataka kuacha kufuatilia taarifa za upotoshaji kwenye mitandao ya kijamii.

“Mkoa wetu umetengewa dozi za Chanjo, 60,000 hadi jana (Agoust 3) tayari zimeletwa dozi 10,000, katika wilaya ya Moshi tumepokea dozi 2700, katika hospitali ya rufaa ya mkoa Mawenzi, tutaweka dozi 500, katika hospitali ya Rufaa  ya Kanda KCMC 500, hii ni  awamu ya kwanza  ila kesho na keshokutwa(Agaoust 4 na 5)tutapokea dozi nyingine,” amesema.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliojitokeza kuchanja katika hospitali ya rufaa ya Mawenzi akimo Sabastin Morio walisema kuwa bado hakuna utaratibu lionadaniwa kwa ajili ya chanjo na kuiomba serikali kuangalia uwezekano kutatua matatizo hayo.

“Ni vyema pia waweke utaratibu wa kuwapima watu  presha na shinikizo la damu kabla ya kuwapatia chanjo hizo, wengine wanaweza kupata madhara kwa sababu tu presha zao  hazikuwa vyema na wakasingizia ni madhara ya chanjo,“ amesema Mary Njau.

Wakati huo huo Nipashe ilitembelea katika hospitali ya rufaa ya kanda KCMC ambapo Mbunge wa Jimbo la Moshi, Priscus Tarimo aliitaka  jamii kutafuta taarifa kutoka vyanzo sahihi kuhusu usalama wa chanjo kwa kuwa katika mitandao ya kijamii, kuna baadhi ya taarifa potofu.

“Nimekuja hapa leo kuchanja kwa sababu natambua umuhimu wa chanjo na tunashukuru serikali kwa kufanya mchakato huu lakini KCMC nao wameweka utaratibu mzuri sana. Shughuli inafanyika kwa weledi na haraka,”

"Tuache kuwatia hofu watanzania na serikali ifanye kila inalowezekana kujibu upotoshaji wowote huo ili sasa suala la kuchanja liwe ni la hiyari ya mtu. Narudia tena tusitiane hofu. Wataalamu wametuhakikishia chanjo ni salama," Tarimo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa KCMC, Gilleard Masenga, amewataka wananchi walioko katika makundi yaliyoorodheshwa katika kipaumbele cha awamu ya kwanza, kujitokeza kuchanja huku akiwahakikisha chanjo ni salama.