Serikali  yamkuna  Waziri Mkuchika  jimboni 

23Jul 2019
Hamisi Nasiri
NEWALA 
Nipashe
Serikali  yamkuna  Waziri Mkuchika  jimboni 

MBUNGE wa Newala Mjini, George Mkuchika, ambaye pia ni Waziri Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi wa Umma na Utawala Bora), ameipongeza serikali kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye jimbo lake ikiwamo ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo iliyojengwa Kata ya Mkunya.

MBUNGE wa Newala Mjini, George Mkuchika.

Mkuchika alitoa pongeza hizo mwishoni mwa wiki mjini Newala alipokuwa akizungumza na wananchi wa kata hiyo ikiwa sehemu ya ziara yake ya kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo.

  Alisema serikali imesikiliza kilio na kero mbalimbali za wananchi wa jimbo hilo kwa kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo imeanza kuleta manufaa kwa wananchi.

“Nikiwa mbunge mara kwa mara nimekuwa nikiiomba serikali kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye jimbo langu, nashukuru imesikia naona miradi mingi inatekelezwa kwa nguvu zote, naipongeza serikali kwa hili,” alisema Mkuchika.

  Mkuchika alisema amefurahishwa na kitendo cha serikali kwa kutekeleza ujenzi wa jengo la mahakama ya mwanzo, na kwamba tayari limeshafikia hatua ya kukamilika na muda wowote kuanzia sasa litaanza kutoa huduma za kimahakama.

   Alisema wananchi wa Kata ya Mkunya moja ya kilio chao kikubwa ilikuwa ni kupatiwa mahakama ili kuwawezesha kusikilizwa kwa madai yao na tayari serikali imeshasikiliza kilio hicho, na kuamua kujenga mahakama hiyo na kwamba kazi ya serikali iliyobaki ni kuharakisha kupeleka wafanyakazi ikiwamo hakimu.

   Alisema wananchi wa Jimbo la Newala Mjini, na hasa Kata ya Mkunya wamekuwa na kero kadhaa za kijamii, afya, maji, barabara na miundombinu mbalimbali, hivyo mara kwa mara wamekuwa wakimweleza mbunge huyo kuwatatulia, lakini sasa baadhi ya huduma wameshaanza kuzipata wakiwa kwenye kata yao.    Mkuchika alisema mahakama hiyo itakapoanza kutoa huduma zake kwa wananchi masuala mengi ya kijamii itakuwa rahisi kuyasikiliza likiwamo suala la mirathi na migogoro mingine inayotokea kwenye jamii.

Habari Kubwa